Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WIZARA ZA UJENZI SMT NA SMZ ZAHIMIZWA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KISEKTA


 

Viongozi na Watendaji wa Wizara ya Ujenzi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), zimehimizwa kuimarisha ushirikiano katika kutatua changamoto za kisera, kisheria na kiutekelezaji zinazojitokeza katika sekta ya ujenzi, kwa lengo la kuleta maendeleo na ustawi wa wananchi wa pande zote mbili.

Akizungumza katika mkutano wa Ushirikiano baina ya Wizara hizo uliofanyika mkoani Arusha, Waziri wa Ujenzi Mhe. Masanja Kadogosa amesema sekta ya ujenzi inahitaji ushirikiano wa karibu kutokana na umuhimu wake katika kuunganisha watu, kufungua fursa za kiuchumi, kuchochea biashara na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii.

Amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kujadili changamoto zilizopo na kubainisha fursa zinazoweza kutumiwa kwa pamoja, huku akiwataka viongozi na wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara hizo kuendeleza mshikamano na kufanya kazi kwa kuzingatia maslahi mapana ya Serikali na wananchi.

Ameeleza kuwa miundombinu inayojengwa ni msingi wa maendeleo ya sasa na ya baadaye, hivyo ni muhimu kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika, usalama na kuzingatia thamani halisi ya fedha zinazotumika.

Aidha, Waziri Kadogosa amesisitiza umuhimu wa wataalamu wa sekta ya ujenzi, hususan wahandisi, wakadiriaji majenzi na wabunifu majengo na taasisi za udhibiti, kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na utaalamu ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inadumu na kuwa salama kwa watumiaji.

Ametoa wito kwa Makatibu Wakuu wa Wizara hizo kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa maazimio yatakayofikiwa katika mkutano huo, kwa kuimarisha uwezo wa sekretarieti ya ushirikiano kufuatilia hatua kwa hatua utekelezaji wa makubaliano katika kila taasisi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar Mhe. Badria Masoud, ameeleza kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu, ikiwemo ujenzi wa barabara ya njia sita, madaraja na barabara za juu zinazolenga kuboresha usafiri na kuimarisha muunganiko wa maeneo mbalimbali.

Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni daraja la kihistoria la Uzi, Barabara ya juu ya Mwanakwerekwe ambayo imekamilika kwa asilimia 100, pamoja na Barabara ya juu ya Amaan ambayo iko katika hatua za mwisho za kukamilika.