Habari
WAZIRI MKUU AAGIZA KASI UJENZI WA BARABARA YA BIGWA–MVUHA-KISAKI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro pamoja na viongozi wa Wakala huo kutoka Makao Makuu kuhakikisha wanasimamia kwa karibu utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Bigwa–Kisaki, sehemu ya Bigwa–Mvuha yenye urefu wa kilometa 78, kutokana na umuhimu wake kiuchumi na kijamii.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Dutumi, Morogoro Kusini, leo Novemba 22, 2026, Waziri Mkuu pia amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha anarejea kazini na kuongeza kasi ya ujenzi mara baada ya kupokea malipo ya madai yake, akieleza kuwa Serikali imeanza kulipa madeni ya makandarasi ili kuwezesha kuendelea kwa miradi iliyokuwa imesimama.
Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa hataki visingizio katika utekelezaji wa mradi huo na kwamba atafuatilia kwa karibu maendeleo yake, ikiwemo kufanya ziara nyingine ya kukagua utekelezaji wa kazi.
"Nimwambie mkandarasi akae mguu sawa. Atakapopata fedha atekeleze kwa kasi mradi huu na hatutaki kisingizio chochote kuhusu mradi huu. Mimi mwenyewe nitakuja tena kuukagua," amesema Dkt. Mwigulu.
Aidha, Dkt. Mwigulu amemuagiza Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, kuhakikisha mkandarasi anaelekezwa kuleta vifaa na wataalamu wa kutosha katika eneo la mradi ili kuharakisha utekelezaji wa ujenzi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya, amewahakikishia wananchi wa Morogoro Kusini kuwa ifikapo wiki ijayo mkandarasi anayejenga barabara hiyo atakuwa amelipwa fedha zake, kama ambavyo Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, alivyomhakikishia Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Mhe. Hamis Taletale.
Mhandisi, Kasekenya ameeleza kuwa barabara hiyo inapita katika maeneo ya uzalishaji wa chakula, kilimo cha viungo na shughuli za uchimbaji madini, hivyo kukamilika kwake kutarahisisha usafirishaji wa mazao na rasilimali hizo.
Naye, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Mhe. Hamis Taletale, ameiomba Serikali kuhakikisha mkandarasi anayetekeleza mradi wa Barabara ya Bigwa–Kisaki analipwa madai yake ya fedha za awali zilizobakia kama alivyoahidiwa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, ili aweze kurejea eneo la mradi na kuendelea na utekelezaji wa ujenzi.
