Habari
DKT. MWIGULU: FEDHA ZA MIRADI ZIPO, MAKANDARASI HAKUNA KISINGIZIO
📌Awataka kukamilisha miradi kwa wakati
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemuagiza Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya kuhakikisha anawatangazia makandarasi wote nchini kukamilisha miradi ya miundombinu kwa wakati, akisisitiza kuwa Serikali kwa sasa inalipa madai ya makandarasi kwa wakati na hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha utekelezaji wa miradi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtongani, Wilayani Kibaha, mkoani Pwani, leo, Novemba 21, 2026, Waziri Mkuu amesema kuwa tangu kuanza kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imekuwa ikitoa fedha na ikielekeza fedha hizo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo ya ujenzi wa barabara.
"Kwa kuwa upo hapa, nataka uwatangazie makandarasi kuwa tunataka kazi zikamilike, hatuna kisingizio. Makandarasi wakishatekeleza kazi watapata malipo yao kwa sababu kwa sasa fedha zipo na zinakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuelekezwa kwenye Mifuko ikiwemo wa Barabara kwa ajili ya utekelezaji wa miradi," amesema Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Mkuu amemuagiza Naibu Waziri huyo kulipa kipaumbele suala la malipo ya awali kwa mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara ya Mlandizi–Ruvu SGR ili kuhakikisha anaendelea na kazi bila kukwama.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema Serikali itajenga barabara ya Makofia–Mlandizi–Mwaneromango yenye urefu wa kilometa 100 kwa kiwango cha lami, kwa lengo la kurahisisha usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani na mikoa jirani.
Ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo umegawanywa katika vipande vitatu na utatekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza itahusisha kipande cha Mlandizi–Ruvu SGR chenye urefu wa kilometa 23, ambacho ni kipaumbele cha Serikali. Amesema mkandarasi tayari amepatikana na yupo eneo la mradi, huku maandalizi ya malipo ya awali yakiendelea.
Ameongeza kuwa usanifu wa vipande vingine vya Makofia–Mlandizi (kilometa 35) na Ruvu SGR–Mwaneromango umekamilika, na kinachosubiriwa ni kukamilika kwa taratibu za ulipaji fidia kwa wananchi watakaopisha miradi hiyo ili ujenzi uweze kuanza.
Kuhusu barabara ya Kongowe–Soga, Mhandisi Kasekenya amesema Wizara ya Ujenzi imepewa jukumu la kuisanifu barabara hiyo, ambayo awali ilikuwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).
Ameeleza kuwa maandalizi ya kuitangaza zabuni yamekamilika ili kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya usanifu wa barabara hiyo.
Naye, Mbunge wa Kibaha Vijijini, Mhe. Hamoud Jumaa, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuwaletea wananchi maendeleo na kuiomba Serikali kuijenga barabara ya Makofia–Mlandizi–Maneromango yenye urefu wa kilometa 100 kwa kiwango cha lami ili kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji katika eneo hilo.
