Habari
KADOGOSA ATOA SIKU 30 KWA TBA KUWASILISHA TAARIFA YA HALI YA NYUMBA ZA SERIKALI NA UKUSANYAJI WA PANGO
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, ametoa siku 30 kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuwasilisha ofisini kwake taarifa ya hali ya nyumba za Serikali nchini pamoja na mwenendo wa ukusanyaji wa kodi ya pango.
Waziri Kadogosa ametoa agizo hilo mkoani Tanga wakati akizungumza na watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi.
Amesisitiza kuwa Serikali haiwezi kuendelea kuwa na madeni ya kodi ya pango kutoka kwenye nyumba zake, hivyo TBA inapaswa kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wapangaji wanalipa kodi kwa wakati na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wanaoshindwa kutekeleza wajibu huo.
Katika hatua nyingine, Waziri Kadogosa ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuongeza kasi ya matengenezo ya barabara, hususan zile zinazounganisha maeneo muhimu ya kiuchumi (Economic Corridors), kwa kuhakikisha mashimo yanazibwa na barabara zinakuwa katika hali nzuri na kupitika wakati wote.
Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara, hivyo hakuna sababu ya barabara kuendelea kuwa na mashimo kutokana na kutofanyika kwa matengenezo ya kawaida.
“Nimewaelekeza mameneja kwamba fedha zinatolewa, hakuna kisingizio. Fedha hizi zimeanza kutoka tangu mwezi Julai, hivyo ni lazima kuhakikisha mashimo yanazibwa na barabara zinakuwa katika hali nzuri,” amesisitiza Kadogosa.
Aidha, Waziri Kadogosa ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kuboresha utoaji wa huduma, hususan katika matengenezo ya magari ya Serikali. Amesisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora wa huduma na gharama za matengenezo ili kuhakikisha thamani ya fedha za umma inapatikana.
Ameeleza kuwa Wizara ya Ujenzi ni miongoni mwa wizara nyeti nchini kutokana na mchango wake katika sekta za usafiri, usafirishaji na maendeleo ya shughuli za kiuchumi. Hivyo, amezitaka taasisi zote zilizo chini ya wizara hiyo kuongeza uwajibikaji na kutekeleza majukumu yao kwa viwango vinavyotarajiwa.
Vilevile, amezitaka taasisi hizo kuendelea kufanya tathmini za utendaji kazi na usimamizi wa vihatarishi (Risk Assessment) ili kubaini changamoto mapema na kuchukua hatua za kuzitatua kabla hazijaathiri utekelezaji wa majukumu yao.
