Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BARABARA KUENDELEA KUKARABATIWA MARA KWA MARA – DKT. MSONDE


Wizara ya Ujenzi imeweka mikakati ya kuhakikisha miundombinu ya barabara nchini inafanyiwa ukarabati na matengenezo ya mara kwa mara ili kuongeza muda wa matumizi yake na kuendelea kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa leo, Novemba 16, 2026, jijini Mwanza na Dkt. Charles Msonde wakati wa Mkutano wa 19 wa Tathmini ya Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi (JTRS) uliofunguliwa na Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba na kuwakutanisha wadau kutoka Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

Dkt. Msonde amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kutathmini maendeleo ya sekta ya miundombinu, kuangalia hatua zilizofikiwa, hali ya sasa na mipango ya baadaye, pamoja na kujadili changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha mwaka mzima na kutafuta suluhisho lake.

Akizungumzia mtandao wa barabara unaosimamiwa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), amesema nchi ina mtandao wa barabara kuu na za mikoa wenye urefu wa zaidi ya kilomita 37,000, ambapo kati ya hizo zaidi ya  kilometa 12,000 ni barabara za lami na nyingine ni za changarawe na udongo.

Amesema jukumu la sekta ya ujenzi ni kuhakikisha barabara ambazo hazijawekewa lami zinaendelea kuboreshwa, huku zile zenye lami zikifanyiwa matengenezo kwa wakati ili kuongeza uimara na muda wa matumizi yake.

Amesisitiza kuwa barabara zina muda maalumu wa matumizi, hivyo zinahitaji kufanyiwa ukarabati wa mara kwa mara ili kuzuia uchakavu na kuhakikisha zinaendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa muda mrefu.

“Barabara zinatakiwa kufanyiwa ukarabati wa mara kwa mara ili ziendelee kudumu kwa muda mrefu, kwa kuwa zina muda maalumu wa matumizi. Hivyo, ili ziendelee kuwa katika hali bora, zinahitaji kuboreshwa na kuimarishwa,” amesema Dkt. Msonde.

Aidha, ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hauishii katika kuweka tabaka la lami pekee, bali huhusisha matabaka mbalimbali yanayojengwa kwa kuzingatia utaalamu ili kuimarisha barabara na kuzuia maji kupenya na kuharibu muundo wake.

Amesema maji ni miongoni mwa visababishi vikuu vya uharibifu wa barabara, hivyo ni muhimu kuzingatia ubora wa matabaka yake pamoja na mifumo ya kuondoa maji ili kuongeza uimara wa miundombinu hiyo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Msonde amesema mtandao wa barabara umegawanywa katika korido tisa kwa lengo la kurahisisha usimamizi, uratibu na utoaji wa huduma za matengenezo.

Pia ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuweka utaratibu wa fedha za matengenezo ya barabara kwenda moja kwa moja kwenye mifuko ya barabara, akieleza kuwa hatua hiyo imesaidia kurahisisha upatikanaji wa fedha na kuongeza kasi ya utekelezaji wa matengenezo.