Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

ICOT YATAKIWA KUONGEZA WATAALAMU WA SEKTA YA UJENZI


Serikali imesema itaendelea kuiimarisha Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT), ili kutayarisha wataalamu wengi wenye ujuzi na umahiri watakaoweza kujiajiri na kuajirika kikamilifu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Balozi, Eng. Aisha Amour amesema hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa mafundi sanifu na wataalamu wa kada mbalimbali za ujenzi watakaosaidia kukabiliana na upungufu wa wataalamu katika miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini na kuchangia kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza katika Mahafali ya Nne ya (ICoT) yaliyofanyika mkoani Morogoro, Katibu Balozi, Eng. Amour, amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika elimu ya ufundi na uhandisi ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na sekta ya ujenzi.

Amesema uwepo wa wataalamu wenye ujuzi wa vitendo ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya ujenzi inatekelezwa kwa ubora, ufanisi na kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

“Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya taasisi hii kwa kufanya ukarabati wa majengo pamoja na kujenga jengo jipya la taaluma lenye ghorofa nne ambalo limefikia asilimia 98 ya ujenzi”, amesema Eng. Amour.

Amesema jengo hilo likikamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1,000 na hivyo kuongeza nafasi za udahili pamoja na kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa vitendo.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo amesema ICoT inatarajia kuongeza programu za mafunzo kutoka tatu zilizopo sasa hadi sita katika mwaka ujao wa masomo, hatua itakayoongeza mara mbili uwezo wa taasisi hiyo kutoa mafunzo na kuzalisha wataalamu wa sekta ya ujenzi.

Jumla ya wanafunzi 308 wamehitimu mafunzo katika mahafali hayo, ambapo 82 wamehitimu ngazi ya Stashahada (Diploma), huku 226 wakihitimu mafunzo ya ufundi stadi katika ngazi za Level II na III.

Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) ni taasisi ya mafunzo iliyo chini ya Wizara ya Ujenzi inayotoa mafunzo katika fani za uhandisi ujenzi, uhandisi umeme na uhandisi mitambo, pamoja na mafunzo ya ufundi stadi na kozi mbalimbali za muda mfupi.

Taasisi hiyo ilianzishwa kwa kuunganisha Chuo cha Ujenzi Morogoro (Morogoro Works Training Institute) na Taasisi ya Teknolojia Stahiki ya Nguvukazi ya Mbeya (Appropriate Technology Training Institute), kwa lengo la kuimarisha utoaji wa mafunzo na kuongeza uzalishaji wa wataalamu wenye ujuzi katika sekta ya ujenzi nchini.