Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KADOGOSA AAGIZA TANROADS KUMUONDOA MSIMAMIZI WA MRADI UWANJA WA NDEGE TANGA


 

📌 Mwakilishi wa Mkandarasi naye akutana na rungu, aagiza aondolewe mara moja kwenye mradi

📌 Ahoji matumizi ya fedha za awali

Waziri wa Ujenzi Mhe. Masanja Kadogosa ameuagiza Wakala ya Barabara Nchini (TANROADS) kumuondoa mara moja Mhandisi anayesimamia mradi wa ujenzi wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha  Ndege mkoani Tanga na kumteua msimamizi mwingine mwenye uwezo wa kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi.

Aidha, Waziri Kadogosa ametoa maelekezo ya kuondolewa kwa Mwakilishi wa Mkandarasi wa Mradi huo kwa kufanya kazi kwa mazoea na kupuuza maelekezo ya Serikali.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo, tarehe 21 Novemba 2026, Waziri Kadogosa amesema pamoja na kuwepo kwa mabadiliko ya wigo wa kazi (scope), bado kuna changamoto katika utekelezaji wa mradi, hali inayohitaji hatua za haraka kutoka kwa pande zote zinazohusika.

Ameeleza kuwa mkandarasi alipaswa kuwa amekamilisha maandalizi ya rasilimali za mradi (mobilization) kwa kiwango cha asilimia 100 mwezi Februari, lakini hadi sasa kiwango cha vifaa na watumishi kimeendelea kuwa chini, hali inayochangia kasi ndogo ya utekelezaji wa kazi.

Aidha, Waziri Kadogosa amehoji matumizi ya malipo ya awali (advance payment) yaliyotolewa kwa mkandarasi kwa ajili ya maandalizi ya mradi, akisisitiza kuwa fedha hizo zinapaswa kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.

 

“Mkandarasi amelipwa advance payment kwa ajili ya mobilization. Kama mobilization haijafanyika kwa kiwango kinachotakiwa, fedha hizo zimetumika wapi? Hili ni suala linalohitaji majibu,” amesema Waziri.

Ameitaka TANROADS kuimarisha usimamizi wa mradi na kuhakikisha watumishi wake wanawajibika ipasavyo, akibainisha kuwa changamoto za mkandarasi hazipaswi kuwa sababu ya upande wa Serikali kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tanga ambaye pia ni mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa Tanga Edwin Methew, amesema ziara hiyo imeonesha mwanga wa maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo, huku akiahidi kuwa changamoto zilizobainika zitafanyiwa kazi kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ubora na kwa wakati.

 kumteua msimamizi mwingine mwenye uwezo wa kusimamia utekelezaji wa mradi kwa ufanisi, kufuatia kubainika kwa changamoto katika usimamizi na kasi ya kazi.