Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WATUMISHI WIZARA YA UJENZI, WAPATIWA ELIMU KUKABILIANA NA HOMA YA INI


Watumishi wa Wizara ya Ujenzi leo, Agosti 28, 2026, wamepatiwa elimu ya afya iliyolenga kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa wa homa ya ini, ikiwemo visababishi, dalili, athari, njia za kujikinga na kudhibiti maambukizi.

Semina hiyo imeendeshwa na wataalamu wa afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ambapo Dkt. Zainab Swedi alitoa takwimu kuhusu ugonjwa wa homa ya ini nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, pamoja na kueleza visababishi na dalili za ugonjwa huo.

Aidha, Dkt. Ngayane Maguha alieleza kuhusu athari za homa ya ini, uhusiano wake na maambukizi ya VVU na UKIMWI, pamoja na hatua muhimu za kujikinga na kudhibiti maambukizi.

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara ya Ujenzi, ni muendelezo wa mafunzo yanayolenga kuongeza uelewa wa watumishi kuhusu masuala ya afya, kuhamasisha hatua za kinga dhidi ya magonjwa na kuimarisha ustawi wao katika maisha ya kila siku.

Semina hiyo ni sehemu ya utaratibu wa Wizara ya Ujenzi wa kutoa elimu ya afya pamoja na masuala mengine kwa watumishi wake kila mwisho wa mwezi, kwa lengo la kujenga jamii ya watumishi wenye uelewa na kuzingatia afya na ustawi katika utendaji wao wa kazi.