Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

DARAJA LA KYANYABASA LAFUNGUA FURSA MPYA, WANANCHI WAIPONGEZA SERIKALI


 

Wananchi wa Tarafa ya Katerero, Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera wameishukuru Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa Daraja la Kyanyabasa, wakisema mradi huo umeleta matumaini mapya na kurahisisha usafiri pamoja na shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

Daraja hilo lenye urefu wa mita 105 na barabara unganishi zenye urefu wa mita 600, limeondoa changamoto ya wananchi kutegemea mitumbwi na kivuko katika kuvuka eneo hilo.

Mkazi wa Kata ya Kishogo, Bw. Proges Mtuli, amesema kukamilika kwa daraja hilo ni hatua kubwa ya maendeleo kwa wananchi, ikizingatiwa kuwa awali walikabiliwa na changamoto mbalimbali wakati wa kutumia mitumbwi.

Amesema mitumbwi hiyo ilikuwa midogo na mara nyingi ilizidiwa na idadi ya abiria, hali iliyoweka maisha ya wananchi hatarini, huku baadhi yao wakianguka majini.

Kwa mujibu wa Mtuli, hata baada ya Serikali kuwaletea kivuko, bado kulikuwa na changamoto kutokana na wingi wa abiria, gharama za usafirishaji na muda wa huduma, ambapo nyakati za jioni shughuli za kuvusha watu zilisimamishwa.

“Tunaishukuru Serikali kwa kukamilisha daraja hili. Sasa wananchi tumepata uhakika wa usafiri na fursa zaidi za kufanya shughuli zetu bila hofu ya changamoto tulizokuwa tukikabiliana nazo awali,” amesema.

Wananchi hao pia wameahidi kushirikiana katika kulinda daraja na barabara unganishi ili miundombinu hiyo idumu na iendelee kutoa huduma kwa vizazi vijavyo.

Kukamilika kwa Daraja la Kyanyabasa kunatarajiwa kuimarisha mawasiliano ya barabara katika tarafa ya Katerero na kuchochea shughuli za kiuchumi, ikiwemo usafirishaji wa abiria, mazao ya chakula na bidhaa za biashara.

Mradi huo unaonekana kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo kwa wananchi wa eneo hilo, huku ukifungua fursa za kiuchumi na kuimarisha uhusiano wa kijamii na kibiashara katika maeneo yanayounganishwa na barabara hiyo.