Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KWAGILWA AIPONGEZA WIZARA YA UJENZI NA TANROADS UHIFADHI WA MAZINGIRA KUPITIA UPANDAJI MITI


Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa, ametembelea na kukagua banda la Wizara ya Ujenzi pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) katika Maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026 yanayofanyika katika Viwanja vya Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Akiwa katika banda hilo leo, Juni 01, 2026 Mhe. Kwagilwa ameipongeza Wizara ya Ujenzi na TANROADS kwa kuendelea kutekeleza utamaduni wa upandaji miti katika miradi ya barabara, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, Kwagilwa amesema kuwa Serikali inaelekea kufanya suala la upandaji miti katika miradi ya maendeleo kuwa la kisheria badala ya kutegemea hiari, ili kuhakikisha kuwa miradi yote inayotekelezwa nchini inaambatana na jitihada za uhifadhi wa mazingira.

“Ni muhimu kuhakikisha kuwa kila mradi wa maendeleo unaenda sambamba na upandaji miti ili kulinda na kuboresha mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema Mhe. Kwagilwa.

Maonesho hayo yameanza leo na kufunguliwa rasmi na Naibu Waziri huyo, huku yakitarajiwa kuhitimishwa Juni 05, 2026 ambapo Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”