Habari
DKT. JAFAR SEIF APONGEZA JUHUDI ZA UHIFADHI WA MAZINGIRA
📌Aahidi kutembelea mradi wa kukijanisha Dodoma
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Sekta ya Afya, Dkt. Jafar Seif, ametembelea na kukagua banda la Wizara ya Ujenzi pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) katika Maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Akiwa katika banda hilo leo, Juni 3, 2026, Dkt. Seif alipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Wizara ya Ujenzi na TANROADS katika kuhifadhi na kutunza mazingira kupitia miradi ya maendeleo ya miundombinu nchini.
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Dkt. Seif alipongeza juhudi zinazofanywa na Wizara pamoja na TANROADS katika kuhakikisha miradi ya barabara inazingatia masuala ya uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, ameahidi kutembelea mradi wa ujenzi wa Barabara ya Mzunguko wa Jiji la Dodoma (Dodoma Outer Ring Road) ili kujionea utekelezaji wa mradi wa kukijanisha jiji la Dodoma (GSP) ambapo miti 97,000 tayari imekwisha pandwa lengo likiwa ni kuhifadhi mazingira na kuimarisha mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026 yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 5, 2026, yakiongozwa na kaulimbiu isemayo: “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”
