Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WAKAZI WA KATERERO NA IBWELA KUNUFAIKA NA DARAJA LA KALEBE, KAGERA


Wakazi wa maeneo ya Katerero na Ibwela mkoani Kagera wanatarajia kunufaika na Daraja la Kalebe, ambalo limejengwa ili kurahisisha usafirishaji na kuimarisha mawasiliano kati ya wilaya za Bukoba, Muleba na Karagwe.

Daraja hilo linatarajiwa kuwa suluhisho kwa wakazi na wafanyabiashara, hususan katika kusafirisha mazao ya biashara kwenda katika masoko mbalimbali. Awali, watumiaji wa eneo hilo walikabiliwa na changamoto kubwa kutokana na daraja la zamani kushindwa kupitika, hasa wakati wa msimu wa mvua.

Msimamizi wa ujenzi wa mradi wa Daraja la Kalebe, Mhandisi Kenneth Mkude, amesema daraja hilo jipya lina urefu wa mita 60 na upana wa mita 11.

Amesema daraja la awali lilikuwa dogo na lilikuwa na uwezo wa kubeba mizigo yenye uzito wa tani 10 pekee, hali iliyokuwa ikikwamisha shughuli za usafirishaji katika eneo hilo.

Aidha, amesema ujenzi wa mradi huo umehusisha uboreshaji wa tuta la barabara pamoja na maungio ya daraja yenye urefu wa kilomita 1.2.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mkude, maboresho hayo yataondoa changamoto ya mafuriko yaliyokuwa yakitokana na maji mengi kupita juu ya daraja wakati wa mvua.

Ameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo, akisema utakuwa fursa kubwa kwa wakazi na watumiaji wengine wa daraja hilo kwa kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.

Hata hivyo, ametoa wito kwa watumiaji wa barabara na daraja hilo kutunza miundombinu iliyowekwa ili kuhakikisha inadumu kwa muda mrefu.

“Ni jukumu la kila mmoja wetu kuwa mlinzi wa mwenzake na kutunza miundombinu hii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema.

Pia amewataka watumiaji wa daraja wanaotembea kwa miguu kuhakikisha wanatumia njia maalumu ya watembea kwa miguu badala ya kupita katika njia inayotumiwa na magari, ili kuepuka ajali.

Ujenzi wa mradi huo umefanywa na kampuni ya wazawa ya Mirembe Construction Co. Ltd, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 100.

Kwa sasa, mkandarasi amekamilisha sehemu ya daraja inayotumiwa na magari na anaendelea na kazi za usafi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo sehemu ya chini ya daraja, kwa kuondoa udongo na vifusi ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi.