Habari
SERIKALI YATOA BILIONI 19 ZA FIDIA KWA WANANCHI ARUSHA
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amesema Serikali imetoa Shilingi Bilioni 19 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa barabara za AFCON 2027 jijini Arusha, huku akitoa maelekezo kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) kuanza malipo hayo mara moja ili kuruhusu ujenzi kuendelea bila vikwazo.
Kadogosa ameyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya miradi ya barabara za AFCON zinazotekelezwa jijini Arusha, akisisitiza kuwa fedha za fidia tayari zimepatikana na hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha malipo kwa wananchi wanaostahili.
Amesema fedha hizo zilizotolewa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zinapaswa kuanza kulipwa ndani ya siku mbili hadi tatu ili wananchi wapate stahiki zao na wakandarasi waendelee na kazi bila kusimama.
Amebainisha kuwa lengo la Serikali si kujenga barabara kwa ajili ya AFCON pekee, bali kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na miundombinu hiyo hata baada ya mashindano kumalizika.
"Tunataka kuona barabara hizi zinazojengwa kwa maandalizi ya AFCON 2027 zikiwa na ubora unaostahili na kuendelea kuwanufaisha wananchi hata baada ya mashindano hayo kumalizika", amesisitiza Kadogosa.
Katika ukaguzi huo, Kadogosa pia ameeleza kuridhishwa na hatua za wakandarasi kujipanga kutekeleza miradi hiyo, pamoja na kuupongeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kupitia Kitengo cha TECU, kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.
Aidha, Kadogosa amesisitiza umuhimu wa mkandarasi kuongeza vifaa, mitambo na nguvu kazi katika maeneo yote ili kuongeza kasi ya ujenzi kwa kufanya kazi saa 24, mchana na usiku, ili kuhakikisha muda uliopo unatumika vizuri na mradi unakamilika kwa wakati.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Arusha Mhandisi Reginald Massawe amemhakikishia Waziri kuwa wakandarasi wamekamilisha kwa asilimia 100 uhamishaji wa vifaa na mitambo katika eneo la miradi pamoja na kuweka wataalamu wanaohitajika. Amesema hatua hiyo imechangia kuongeza kasi ya utekelezaji wa kazi, ambazo zinaendelea kufanyika mchana na usiku.
Naye, Msimamizi wa Mradi wa Barabara ya Mbauda–Losinyai yenye urefu wa kilometa 70 kutoka TECU, Mhandisi Hophine Mollel, amesema kipande cha kilometa 13 kinachotekelezwa kwa ajili ya maandalizi ya AFCON 2027 kimefikia asilimia 54.4 ya utekelezaji.
