Habari
SERIKALI KUJENGA BARABARA YA MIKUMI–KILOSA KWA KIWANGO CHA LAMI
Serikali imesema ipo katika mpango wa kujenga barabara ya Mikumi–Kilosa yenye urefu wa kilometa 72 kwa kiwango cha lami ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi katika Mkoa wa Morogoro na mikoa jirani.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Mikumi Day, Mikumi, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro, leo Novemba 23, 2026.
Mhandisi Kasekenya amesema Mikumi ni eneo muhimu katika mtandao wa barabara nchini, kwani linatarajiwa kuwa moja ya vituo vikubwa vya kuunganisha barabara kutoka Magharibi, Kusini na Kaskazini mwa nchi, hali itakayorahisisha mawasiliano na usafirishaji wa watu na bidhaa katika maeneo mbalimbali.
Ameeleza kuwa mpango wa ujenzi wa barabara hizo unatekelezwa kwa awamu, ambapo ujenzi wa barabara ya Dumila–Kilosa yenye urefu wa kilometa 65 umekamilika, huku sehemu ya barabara kutoka Kilosa–Mikumi yenye urefu wa kilometa 72 usanifu wake ukiwa umekamilika na kwa sasa Serikali inaendelea na hatua za kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi wake.
Vilevile, amesema Serikali ina mpango wa kuifumua na kuijenga upya barabara ya Mikumi–Kidatu yenye urefu wa kilometa 35 kwa kiwango cha lami ili kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji katika eneo hilo.
Kwa upande wao, Mbunge wa Mikumi, Mhe. Dennis Londo, na Mbunge wa Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi, wameiomba Serikali kuipa kipaumbele barabara ya Mikumi–Kilosa kwa kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuondoa changamoto za usafiri na usafirishaji zinazowakabili wananchi wanaotumia barabara hiyo.
