Habari
KADOGOSA AIPONGEZA TBA KWA KUANZA UJENZI WA MAKAZI KALOLENI, AITAKA IJITEGEMEE KIBIASHARA
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, ameupongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa makazi ya watumishi wa umma katika eneo la Kaloleni, jijini Arusha, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza upatikanaji wa makazi bora na kuimarisha uwekezaji wa taasisi hiyo.
Kadogosa ametoa pongezi hizo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo, ambapo ameridhishwa na hatua iliyofikiwa na kusisitiza umuhimu wa TBA kutumia fursa zilizopo kuimarisha uwezo wake wa kifedha na kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha, Waziri Kadogosa ameitaka TBA kubadili mtazamo wa uendeshaji kwa kuanza kutekeleza miradi yake kwa misingi ya kibiashara badala ya kuendelea kutegemea fedha za Serikali.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mfumo wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP), akieleza kuwa mwelekeo huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza uwekezaji na kupunguza utegemezi wa fedha za umma.
Ameeleza kuwa TBA ina mtaji mkubwa kupitia mali na majengo inayomiliki, hivyo inapaswa kufanya tathmini ya mali hizo ili kubaini thamani yake halisi na kuzitumia kama dhamana katika taasisi za kifedha kwa ajili ya kupata mitaji ya kuendeleza miradi mbalimbali.
"Tathmini iliyofanyika awali ilionyesha kuwa mali za TBA zilikuwa na thamani ya takribani shilingi trilioni 1.45. Hata hivyo, thamani hiyo inaweza kuongezeka zaidi baada ya kufanya tathmini inayozingatia kupanda kwa thamani ya maeneo na majengo," ameeleza Kadogosa.
Ameongeza kuwa kupitia tathmini hiyo, mizania ya kifedha ya TBA inaweza kuimarika na kufikia zaidi ya shilingi trilioni tatu au hata trilioni nne, hali itakayoiwezesha Taasisi hiyo kupata mikopo kutoka benki na kuwekeza katika miradi mipya ya ujenzi.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), FRV. Said Rajab Mndeme (ndc), amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa majengo manne yatakayokuwa na uwezo wa kuhudumia familia 56, ambapo kila jengo litakuwa na uwezo wa kuhudumia familia 14.
Amesema kwa sasa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo unaendelea kwa kujenga jengo la ghorofa sita, ambalo limefikia asilimia 43 ya utekelezaji.
Kwa upande wake, Meneja wa TBA Mkoa wa Arusha, Arch. Steven Simba, amesema mradi huo ulianza kutekelezwa mwezi Agosti 2025 na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei 2027, kwa gharama ya shilingi bilioni 6.2.
