Habari
KADOGOSA: MIRADI MIKUBWA NI ALAMA YA UONGOZI IMARA
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amesema utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ni ishara ya uongozi imara unaolenga kuleta matokeo na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
Kadogosa ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Jangwani jijini Dar es Salaam, ambapo amepongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo.
Amesema Daraja la Jangwani ni miongoni mwa ahadi zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa kampeni na kuungwa mkono na wananchi kutokana na umuhimu wake kwa wakazi wa Dar es Salaam.
“Mheshimiwa Rais wakati anafungua kampeni Kawe, katika vitu alivyozungumza na akashangiliwa sana ni pale alipozungumzia ujenzi wa Daraja hili la Jangwani ambalo tunaliona,” amesema.
Waziri Kadogosa ameupongeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na mkandarasi kwa hatua iliyofikiwa, huku akisisitiza umuhimu wa kukamilisha mradi huo kwa wakati, kwa mujibu wa masharti ya mkataba.
“Mkandarasi umefanya kazi nzuri sana. Endelea kufanya kazi kwa juhudi na hakikisha kuwa mradi huu unakamilika ifikapo mwisho wa mwaka 2027,” amesema Kadogosa.
Aidha, amepongeza utaratibu wa kuzalisha na kuandaa baadhi ya vifaa vya ujenzi ndani ya eneo la mradi, akisema hatua hiyo inasaidia kuokoa muda na gharama za usafirishaji wa vifaa kutoka maeneo ya mbali.
Kadogosa amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kujiandaa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua, ikiwemo kuweka makalavati, madaraja ya muda na vifaa vingine muhimu ili kuhakikisha barabara kuu haziathiriwi na mvua.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema Daraja la Jangwani lina umuhimu mkubwa katika shughuli za kitaifa, kisiasa, kidini na kijamii, lakini eneo hilo limekuwa likikabiliwa na changamoto za mafuriko wakati wa mvua kubwa.
Amesema kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kutasaidia kupunguza changamoto hizo, kuboresha mazingira na kurahisisha usafiri kwa wananchi.
Naye, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal (Shetta), ameipongeza Serikali kwa kuwekeza katika eneo hilo, huku akimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kulipa Daraja la Jangwani kipaumbele.
Awali, Meneja wa Ujenzi wa mradi huo, Eng. Leonard Ngayungi, amesema ujenzi umefikia asilimia 43 na unahusisha ujenzi wa daraja pamoja na miundombinu ya watembea kwa miguu.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuboresha usafiri, kupunguza athari za mafuriko na kuongeza ufanisi wa matumizi ya barabara hiyo.
