Habari
ZINGATIENI MAADILI KUBORESHA UTENDAJI KAZI: BALOZI AISHA

Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Balozi, Mhandisi Aisha Amour ameitaka Bodi ya Usajili ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), kuhakikisha inazingatia maadili, haki na weledi katika utendaji kazi ili kupunguza malalamiko.
Mhandisi, Amour ameyasema hayo leo Septemba 17,2025 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa 12 wa Baraza la Wafanyakazi la Bodi hiyo na kusisitiza kuepuka kufanya kazi binafsi za kitaalamu ambazo zina mgongano wa kimaslahi na majukumu yanayotekelezwa na Bodi kwani kufanya hivyo kunapelekea kudumaza na kuzoretesha utendaji wa taasisi.
“Kila mtumishi wa Bodi hii ahakikishe anatimiza wajibu wake kwa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na kanuni za Utumishi wa Umma, pia Menejimenti na Watumishi muwe kitu kimoja katika kujenga Bodi hii”, amesema Balozi Amour.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati na Ujenzi (TAMICO), Tawi la AQRB Arch. Barnabas Gulaka amesisitiza kuwa TAMICO itaendelea kushirikiana bega kwa bega na watumishi kwa mujibu wa sheria na kanuni na kuhakikisha kuwa kila mtumishi anapata stahiki zake kwa mujibu wa Sheria.
Mkutano wa 12 wa Baraza la Wafanyakazi wa AQRB umeshirikisha wajumbe mbalimbali kutoka AQRB, lengo ni kujadili changamoto zinazokabili Bodi hiyo ili kuzitafutia ufumbuzi kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi wa taasisi hiyo.