Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

SERIKALI KUUNGANISHA MKOA WA MBEYA NA NJOMBE KUPITIA MAKETE KWA BARABARA YA LAMI


Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imesema imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mbalizi–Shighamba–Kikondo kwa lengo la kuunganisha na Mkoa wa Mbeya na Njombe kupitia Wilaya ya Makete.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi, Godfrey Kasekenya Bungeni Februari 04, 2026 na Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya alipokuwa akijibu swali la Mheshimiwa Patali Shida Patali, Mbunge wa Mbeya Vijijini, aliyehoji ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mbalizi - Shighamba - Isyonje - Kikondo.

Aidha, Eng. Kasekenya amefafanua kuwa kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa sehemu ya Mlandizi – Santilya (km 10).

Ameeleza kwa upande wa barabara ya Isyonje - Kikondo (km 22) ambayo ni sehemu ya barabara ya Isyonje - Kikombo - Makete (km 96.2) ujenzi kwa kiwango cha lami unaendelea kwa sehemu ya Makete - Iniho (km 36.3) na utekelezaji wake umefikia asilimia 28. 

Katika hatua nyingine, Eng. Kasekenya amefafanua kuwa barabara ya mchepuo (bypass) ya Iwambi–Mbalizi tayari imeboreshwa na magari yameanza kupita na kuongeza kuwa mpango uliopo ni kuijenga kwa kiwango cha lami.

Pia, Eng. Kasekenya amemtaka Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa kuwasilisha taarifa kuhusu changamoto iliyojitokeza kwa mkandarasi anayejenga barabara ya Kinyanambo A hadi Lujewa (kilometa 1.2) katika Halmashauri ya Mafinga ambaye aliondoka eneo la mradi pasipo taarifa.