Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

LIPENI WATU WANACHOSTAHILI: ULEGA


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameagiza wakandarasi nchini kulipa watumishi wao kwa mujibu wa sheria za nchi na si kuwapunja.

Waziri huyo ametoa maelekezo hayo wakati akikagua maendeleo ya barabara ya Same- Kisiwani- Mkomazi yenye urefu wa kilometa 100.5 ambayo inajengwa na mkandarasi M/S China Communication Construction Companya Ltd.

Katika tukio hilo alipata malalamiko kuwa wafanyakazi kwenye ujenzi wanalipwa fedha kidogo kuliko kile kinachokubalika kisheria.

“Hii haikubaliki. Kuna viwango ambavyo tumekubaliana kwa mujibu wa sheria zetu. Ni lazima wakandarasi wote wafuate viwango hivyo. Hilo halina mjadala; alisema Ulega huku akishangiliwa na wafanyakazi hao.

Ingawa Msimamizi wa kampuni hiyo alimuahidi Waziri Ulega kuwa suala hilo litafanyiwa kazi, Waziri Ulega alisema kwamba atalifikisha suala hilo kwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ili wamiliki wa kampuni hiyo waitwe nchini na kukubali rasmi kufuata sheria za Tanzania kwenye malipo.

Katika hotuba yake baada ya ukaguzi huo, Ulega pia alieleza kutofurahishwa na kusuasua kwa mradi huo ulioanza  kutekelezwa tangu mwezi Januari mwaka jana.

"Nilimkabidhi mwenyewe mradi huu Mkandarasi mwaka jana, nimetembelea na kuuona, ukweli ni kwamba bado mkandarasi kasi yake ni ndogo hairidhishi na haifurahishi”, amesema Ulega.

Ameongeza kuwa Serikali inataka kuona  kuwa  barabara hiyo inakamilika kwa wakati na ubora ili isaidie kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi.

Amewahakikishia wananchi wa Same kuwa ujenzi wa barabara hiyo utaenda sambamba na ujenzi wa vituo pamoja na uwekaji wa taa za barabarani kwa ajili ya kuleta mwanga ili kuchochea shughuli za kibiashara katika  maeneo yao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema kuwa kiu ya wananchi wa Same ni kuona barabara hiyo inakamilika ili kuweza kurahisisha shughuli za kiuchumi na kuleta maendeleo katika wilaya hiyo na Taifa kwa ujumla

  Mradi huo umefika asilimia 7 na unagharamiwa na Serikali.