Habari
KASEKENYA: SERIKALI KUENDELEA KUKAMILISHA UJENZI WA BARABARA TANGA - PANGANI - MAKURUNGE (KM 256)
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya ameeleza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani – Saadani hadi Makurunge (km 256) kwa kiwango cha lami ili kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji katika Ukanda wa Pwani.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo unatekelezwa kwa awamu nne ambapo awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani (km 50) umefikia asilimia 77, awamu ya pili ya ujenzi wa Daraja la Mto Pangani pamoja na barabara unganishi (km 14) ujenzi wake umefikia asilimia 80.16 na awamu ya tatu ya ujenzi wa barabara ya Tungamaa – Mkwaja – Kwamsisi – Mkange (km 92.5), ujenzi umefikia asilimia 57.38.
Aidha, amebainisha kuwa sehemu ya nne iliyobaki ya Mkange – Makurunge (km 75) usanifu umekamilika na Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuanza ujenzi wa barabara hiyo.
Eng. Kasekenya ameeleza hayo wakati akijibu swali Bungeni la Mheshimiwa Kassimu Amari Mbaraka, Mbunge wa Tanga Mjini linalosema ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani – Saadani hadi Makurunge kwa kiwango cha lami.
