Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WIZARA YA UJENZI YASHIKA NAFASI YA NNE TUZO ZA UHASIBU


Wizara ya Ujenzi kupitia Kitengo cha Fedha na Uhasibu imeibuka mshindi wa nne katika tuzo za umahiri wa uandaaji bora wa taarifa za hesabu kwa mwaka 2025, katika kundi la Wizara za Serikali.

Tuzo hizo zimetolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), chini ya Wizara ya Fedha, kwa kutambua taasisi na mashirika ya umma na binafsi yanayofanya vizuri katika uandaaji wa taarifa za fedha kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uhasibu katika sekta ya umma (IPSAS).

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Afisa Mwandamizi, CPA Jane Changamike amekipongeza Kitengo cha Fedha na Uhasibu pamoja na watumishi wote wa Wizara kwa kujituma, weledi na ushirikiano uliofanikisha mafanikio hayo.

Amesema tuzo hiyo ni uthibitisho wa dhamira ya Wizara katika kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya usimamizi wa fedha za umma, huku ikiimarisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za Serikali.

Aidha, amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri baina ya watumishi, nidhamu katika utendaji kazi pamoja na usimamizi madhubuti wa rasilimali zinazotolewa kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Wizara.

Tuzo hiyo imepokelewa katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa APC, Bunju, jijini Dar es Salaam, na Afisa Mwandamizi CPA Jane Changamike kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour.

Mafanikio hayo yanaonesha dhamira ya Wizara ya Ujenzi katika kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, uwazi na uwajibikaji kupitia uandaaji wa taarifa sahihi za hesabu zinazozingatia viwango vinavyotambulika kimataifa.