Habari
WALIOJENGA KWENYE HIFADHI ZA BARABARA KUBOMOLEWA BAADA YA SIKU SABA.
Wizara ya Ujenzi imetoa siku saba kwa wananchi waliojenga ndani ya maeneo ya hifadhi ya barabara kuondoa majengo yao kwa hiari, kabla ya kuanza kwa zoezi la ubomoaji kwa wale watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa wakati alipokuwa katika ziara ya kikazi Mkoani Manyara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara Mkoani humo.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Waziri Kadogosa amesisitiza kuwa hakuna mwananchi aliye juu ya sheria, akieleza kuwa maeneo ya hifadhi ya barabara yanapaswa kulindwa na kuheshimiwa kwa mujibu wa sheria zilizowekwa na kupitishwa na mamlaka husika.
Amesema Serikali haitasita kuchukua hatua za kubomoa majengo yaliyojengwa ndani ya maeneo hayo baada ya muda wa siku saba kumalizika, huku akibainisha kuwa fidia italipwa pale ambapo taratibu za kisheria zitakapohalalisha kufanya hivyo.
Aidha, Ameeleza kuwa kulindwa kwa maeneo ya hifadhi ya barabara ni muhimu katika kuwezesha mipango ya upanuzi wa miundombinu ya usafiri siku zijazo, ikiwemo ujenzi wa barabara zenye njia nne na sita.
Amesema endapo maeneo hayo yataendelea kuvamiwa kwa ujenzi holela, utekelezaji wa miradi mikubwa ya barabara utakuwa na changamoto kutokana na kukosekana kwa nafasi ya kutosha.
