Habari
WAZIRI MKUU: SERIKALI YAENDELEA KUIFUNGUA IFAKARA KWA MIRADI YA BARABARA
Serikali imesema itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara, ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii pamoja na kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji nchini.
Hayo yameelezwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Tangini, Ifakara, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro, jana Novemba 25, 2026.
“Ukiangalia hali ilivyo katika wilaya zote za bondeni, kama Ulanga, Malinyi na Mlimba, utatambua kuwa tatizo kubwa ni barabara. Niwahakikishie kuwa tatizo hili tunalifahamu na tumeanza kulishughulikia,” amesema Waziri Mkuu.
Ameeleza kuwa mapema leo asubuhi, akiwa katika ziara yake wilayani Mlimba, alimuagiza mkandarasi anayejenga barabara ya Ifakara–Mbingu yenye urefu wa kilometa 62.5 kuhakikisha anaanza kazi ya ujenzi ndani ya siku 30 ili kuondoa changamoto ya usafiri na usafirishaji inayowakabili wananchi wa eneo hilo.
Aidha, amesema amemuelekeza Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, kuhakikisha malipo ya awali kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 37.3 kutoka Ifakara hadi Chita yanafanyika, pamoja na barabara za Malinyi na Mahenge, ili kuwawezesha wakandarasi kuanza kazi na kuifungua Ifakara na wilaya za jirani pamoja na Mkoa wa Morogoro kwa ujumla.
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa wakandarasi wanapaswa kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi zinatumika kutekeleza kazi zilizokusudiwa, huku akiwataka kuwajibika kwa kuanza na kuendeleza kazi badala ya kutembelea maeneo ya miradi bila kufanya utekelezaji.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema Serikali inaendelea na mpango wa kuifungua Ifakara kupitia ujenzi wa miundombinu ya barabara, kutokana na eneo hilo kuwa kitovu cha utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii kwa wilaya za pembezoni mwa Mkoa wa Morogoro.
Amesema barabara ya Ifakara–Malinyi hadi Songea yenye urefu wa kilometa 112 ni miongoni mwa barabara ambazo Serikali imepanga kuzifanyia kazi kwa utaratibu wa kawaida, ambapo mkataba tayari umesainiwa na kinachosubiriwa ni upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wake kwa kiwango cha lami.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali ina mpango wa kujenga jumla ya kilometa 100 za barabara katika eneo hilo, ambapo kwa kipande cha kilometa 62.5 mkandarasi tayari amelipwa fedha zote za awali, huku kwa kipande cha kilometa 37.5 kutoka Mbingu hadi Chita, maelekezo yametolewa ili mkandarasi alipwe fedha za awali na kuanza kazi.
Naye, Mbunge wa Kilombero, Mhe. Abubakar Assenga, ameipongeza Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa barabara ya Ifakara–Kidatu, akisema imechangia kuchochea shughuli za kiuchumi wilayani humo.
Hata hivyo, ameiomba Serikali kuendelea kuifungua Ifakara na wilaya zinazoizunguka kwa miundombinu bora ya barabara, pamoja na kuimarisha mawasiliano na mikoa jirani ya Ruvuma, Njombe na Lindi.
