Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WAZIRI MKUU Dkt. NCHEMBA ARIDHISHWA UJENZI KIWANJA CHA NDEGE CHA SUMBAWANGA


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba ameipongeza Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Rukwa kwa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Sumbawanga kwa ubora.

Amesema hayo leo alipokagua maendeleo ya ujenzi huo na kusisitiza kuwa kiwanja hicho kimejengwa kwa viwango vya kisasa.

"Hongereni wana Rukwa kwa kupata kiwanja cha ndege cha kisasa kitakachochochea fursa nyingi za kiuchumi", amesema Dkt. Nchemba.

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amesema ujenzi wa kiwanja cha ndege hicho unaotekelezwa na mkandarasi M/s Beijing Construction Engineering Group Co Ltd kutoka China umefikia asilimia 96 na utakamilika ifikapo April mosi mwaka huu.

"Tumejipanga kuhakikisha tunawakabidhi kiwanja hiki wenzetu wa Uchukuzi kiwanja hiki kikiwa kimekamilika ifikapo April mosi", amesisitiza Naibu Waziri Eng. Kasekenya.

Eng. Kasekenya amesema kazi ya ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege, barabara za viungio, maegesho ya ndege na jengo la abiria imekamilika.

Nae Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile amesema wako tayari kukipokea kiwanja hicho mapema mwezi ujao ili kuanza kutoa huduma za ndege mkoani humo.

Kiwanja cha ndege cha Sumbawanga ambacho kilijengwa mwaka 1945 na kukarabatiwa mwaka 1985 kimefanyiwa uboreshaji mkubwa na wa kisasa utakaowezesha ndege za saizi ya kati kutumia kiwanja hicho ambapo zaidi ya shilingi bilioni 60 zimetumika.