Habari
WAZIRI MKUU DKT. MWIGULU AKAGUA UJENZI BARABARA NTYUKA - MVUMI - KIKOMBO
📌Serikali kuendelea kuboresha miundombinu kurahisisha uzalishaji na huduma bora
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amekagua ujenzi wa barabara ya Ntyuka–Mvumi–Kikombo (km 76) pamoja na kipande cha barabara ya Chololo–Mapinduzi (Makao Makuu ya TPDF) chenye urefu wa kilomita 5, inayojengwa kwa kiwango cha lami katika Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Dkt. Mwigulu amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara mkoani Dodoma ili kurahisisha shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma za kijamii. Ameelekeza mradi huo ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
"Utekelezaji wa mradi huu ni sehemu ya dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia ya kuacha alama ya kudumu kwa wananchi kwa kuwa utachochea uzalishaji wa kiuchumi katika Mkoa wa Dodoma", ameeleza Dkt. Mwigulu.
Aidha, amewataka wakandarasi wote nchini kulinda haki za mafundi na vibarua kwa kuhakikisha wanalipwa kwa wakati, akionya kuwa mkandarasi yeyote atakayeshindwa kutekeleza hilo hatapewa kazi nyingine za Serikali.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema utekelezaji wa barabara hiyo ni muhimu kwa ukuaji wa jiji la Dodoma, kwani itaunganisha maeneo muhimu na kuboresha huduma za afya, hususan katika Hospitali ya Macho ya Mvumi.
Ameongeza kuwa Wizara yake itasimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo, ikiwemo kufunga taa za barabarani kulingana na maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha miradi yote ya barabara inakuwa na miundombinu ya taa.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Miradi kutoka TANROADS, Mhandisi Japherson Nnko, amesema mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza yenye urefu wa kilomita 25 kuanzia Ntyuka–Mvumi–Makulu na Kikombo–Chololo–Mapinduzi imefikia asilimia 80.9 na inatekelezwa na kampuni ya China Henan International Corporation Company kwa gharama ya shilingi bilioni 38.199.
Awamu ya pili yenye urefu wa kilomita 53 (Ntyuka–Mvumi Hospitali–Kikombo) imeanza na imefikia asilimia 5.2 ya utekelezaji, ikitekelezwa na kampuni ya China First Highway Engineering Co. Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 98.488.
Mradi huu unaotekelezwa na TANROADS unafadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo umefanikiwa kutoa fursa za ajira zaidi ya wafanyakazi 500 wa Kitanzania katika awamu zote mbili.
