Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WAZIRI BASHUNGWA AITAKA TEMESA KUJIENDESHA KIBIASHARA


Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa, ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kuja na mikakati itakayouwezesha Wakala huo kufanya kazi kibiashara ili kuleta tija katika utendaji kazi wake.

Akizungumza mara baada ya kukutana na Menejimenti ya wakala huo Mhe Bashungwa amesema huu sio wakati wa TEMESA kulalamika na kusononeka, ni wakati wa kujali wateja na kushindana katika soko ili kupata wateja wengi na kuhudumia sehemu kubwa ya jamii kwenye upande wa umeme, eletroniki, mitambo uendeshaji wa vivuko na utengenezaji wa magari.

‘’Namshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa fedha za kutosha za kusimamia miradi yenu, hivyo hakikisheni mnazitumia fedha hizo kwa uaminifu na uadilifu na kuhakikisha miradi ya ujenzi mnayoendelea nayo hususani ya vivuko na huduma za ufundi wa umeme na magari inakamilika kwa wakati,’’amesema Mhe. Bashungwa.

Waziri huyo wa Ujenzi amewataka wafanyakazi wote wa TEMESA kufanya kazi kwa mtazamo chanya utakaovutia jamii kubwa ya Watanzania kutumia huduma za TEMESA ambazo zitakuwa bora, za uhakika na za kuaminika badala ya kwenda kupata huduma hizo kwenye taasisi zingine.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ujenzi, Mhandisi Balozi Aisha Amour, amemhakikishia Waziri wa Ujenzi kuwa TEMESA iko kwenye mkakati wa mabadiliko katika utendaji na ukusanyaji wa mapato ili kuhakikisha mapato yote yanayopatikana yanakusanywa kwa wakati.

Mtendaji Mkuu wa TEMESA Lazaro Kilahala, amesema kuwa maelekezo yote na miongozo iliyotolewa na Wizara itafanyiwa kazi na kuelekezwa kwa watumishi wote wa Wakala huo nchini.

Waziri Bashungwa alikua katika ziara ya kukutana na Menejimenti ya TEMESA ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipoteuliwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwa Waziri wa Ujenzi.