Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

RAIS Dkt. SAMIA KUIFUNGUA RUKWA KIMIUNDOMBINU


 

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuifungua nchi kimiundombinu ili kuchochea uzalishaji na biashara mipakani.

Akizungumza na wakazi wa Namanyere Wilayani Nkasi  katika ziara ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba inayoendelea mkoani Rukwa Eng. Kasekenya amesema Rais Dkt. Samia ameamua kuwekeza kwenye barabara ili kuwezesha wananchi kufanya shughuli za kijamii na kiuchumi kwa haraka, uhakika na unafuu zaidi.

"Mkoa wa Rukwa ni mkoa wa kimkakati hivyo tumeelekezwa kuwa uwekezaji katika ziwa Tanganyika uendane na ujenzi wa barabara ili kurahisisha huduma za usafiri na uchukuzi na hivyo kuchochea uchumi wa wananchi", amesisitiza Eng. Kasekenya.

Eng. Kasekenya amesema Wizara ya Ujenzi imepanga kuzijenga kwa lami barabara za Laela-Kizombwe-Kaseesya km 136.8, Namanyere - Katongoro-Kapili Port km 64.80 na Lyazumbi- Kabwe km 63.85 kwa lami ili kuchochea biashara kati ya Tanzania, DRC na Zambia.

Amezitaja barabara nyingine zitazojengwa ili kuufungua ukanda wa magharibi mwa Tanzania kuwa ni Kibaoni – Mpanda (Stalike) km 71, Mpanda-Mishamo km 100 na Mishamo-Uvinza km 86.