Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KAMATI YA MIUNDOMBINU YAAGIZA USIMAMIZI MADHUBUTI UJENZI WA JENGO LA TAALUMA LA ICoT.


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuhakikisha inamsimamia kwa karibu mkandarasi anayejenga jengo la taaluma katika makao makuu ya Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) ili mradi huo ukamilike kwa ubora unaotakiwa.

Agizo hilo limetolewa Mkoani Morogoro leo Machi 12, 2026 na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Prof. Joyce Ndalichako, baada ya wajumbe wa Kamati hiyo kukagua na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo ambao umefikia asilimia 74 ya utekelezaji.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Prof. Ndalichako ameeleza kuwa Kamati inaipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuendeleza chuo hicho kupitia mradi huo muhimu, akisisitiza kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutaimarisha utoaji wa huduma za kitaaluma na kuongeza idadi ya wataalamu wa fani za ujenzi nchini.

Ameongeza kuwa Kamati itaendelea kushirikiana na Wizara ya Ujenzi kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa ubora unaozingatia masharti ya mkataba.

Awali akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi huo mbele ya Kamati, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega, ameeleza kuwa Wizara imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo la ghorofa nne (4) litakalokuwa na ofisi za idara za kitaaluma pamoja na madarasa yatakayoweza kuhudumia wanafunzi takribani 1,000 kwa wakati mmoja ili likamilike na liweze kutoa huduma iliyokusudiwa.

Aidha, Waziri Ulega ameishukuru Kamati hiyo kwa kuibua wazo la ujenzi wa jengo hilo na kwa kuendelea kufuatilia maendeleo ya Taasisi hiyo ili kuhakikisha inatimiza malengo ya kuongeza wataalamu wenye ujuzi katika Sekta ya Ujenzi.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, ameipongeza Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya Chuo hicho, ikiwemo kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo la taaluma.

Mradi wa ujenzi wa jengo la taaluma la ICoT unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 5.978 na kutekelezwa na Mkandarasi Mzawa B.H. Ladwa na kusimamiwa na Mhandisi Mshauri Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).