Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WATUMISHI WIZARA YA UJENZI WAPATIWA ELIMU YA UWEKEZAJI


Watumishi wa Wizara ya Ujenzi wamepatiwa elimu kuhusu fursa za uwekezaji kupitia mfuko wa uwekezaji wa pamoja unaosimamiwa na Shirika la Nyumba la Watumishi chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Semina hiyo imefanyika leo, Septemba 25, 2026, katika Ofisi za Wizara ya Ujenzi, jijini Dodoma na kuendeshwa na wataalamu kutoka Shirika hilo kwa lengo la kuwaongezea watumishi uelewa kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji na umuhimu wa kuweka akiba kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.

Akizungumza katika semina hiyo, mtaalam wa wa masuala ya Uwekezaji kutoka Shirika hilo. Bw. Jafary Yakubu, ameelezea kuhusu Mfuko wa Faida (Faida Fund), ambao unalenga kutoa fursa ya uwekezaji kwa Watanzania na taasisi kupitia ununuzi wa vipande vya uwekezaji, kwa lengo la kupata mapato yanayotokana na ukuaji wa mitaji na kukuza utamaduni wa kuwekeza katika masoko ya fedha na mitaji.

Aidha, ameeleza sababu za kuwekeza kupitia mfuko huo pamoja na namna ya kujiunga na kupata huduma hizo kupitia njia mbalimbali, ikiwemo programu ya simu, tovuti na menyu ya simu.

Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha watumishi kuwa na uelewa mpana kuhusu masuala ya uwekezaji na kuwahamasisha kujiwekea akiba pamoja na kutumia fursa mbalimbali za uwekezaji kwa ajili ya kujenga ustawi wao wa kifedha.

Semina hiyo ni sehemu ya utaratibu wa Wizara ya Ujenzi wa kutoa elimu kwa watumishi wake kuhusu masuala mbalimbali kila mwisho wa mwezi, ikiwa ni hatua ya kuongeza uelewa, maarifa na uwezo wa watumishi katika masuala yanayogusa maisha yao ya kila siku.