Habari
WATUMISHI WAPYA WIZARA YA UJENZI WAPEWA SEMINA ELEKEZI
Watumishi wapya wa Wizara ya Ujenzi wametakiwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kuwajibika katika maeneo yao ya kazi na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, ili kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi katika utendaji wa Wizara.
Wito huo umetolewa Mkoani Singida na Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi wa umma kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tawi la Singida, Bw. Lameck Sospeter Kashaija wakati akifungua mafunzo elekezi ya awali (Induction Course) kwa watumishi wapya wa Wizara ya Ujenzi.
Mafunzo hayo ya siku tano yanalenga kuwajengea watumishi hao uelewa kuhusu majukumu yao, taratibu za utumishi wa umma, maadili na namna bora ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Vilevile, mafunzo hayo yanatarajiwa kuwawezesha watumishi hao kuanza majukumu yao wakiwa na uelewa mpana wa mazingira ya utumishi wa umma na wajibu wao katika kuhakikisha Wizara ya Ujenzi inatoa huduma bora kwa wananchi.
Jumla ya watumishi wapya 35 wanashiriki mafunzo hayo.
