Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BARABARA YA KAHAMA–ULYAHULU JUNCTION–KAKOLA KUUNGANISHA SHINYANGA, GEITA NA KAGERA


Barabara ya Kahama–Ulyahulu Junction–Kakola yenye urefu wa kilomita 73, inayojengwa kwa kiwango cha lami, inatarajiwa kuunganisha Manispaa ya Shinyanga na mikoa jirani ya Geita na Kagera, huku ikifungua fursa za kiuchumi na kijamii katika maeneo itakayopita.

Mhandisi John Kalando, Msimamizi wa Kitengo cha Miradi ya Maendeleo wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga, ameeleza hayo wakati akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya mradi huo wa kimkakati.

Kwa mujibu wa Mhandisi Kalando, ujenzi wa barabara hiyo unaanzia eneo la Manzese kupitia Kahama, Ilogi hadi Kakola, na kwa sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 88.1, ambapo kilomita 36.075 tayari zimewekewa lami.

Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kuongeza fursa katika sekta za kilimo, madini, ufugaji na mazao ya misitu, pamoja na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa.

Mradi huo unaotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ufadhili wa Kampuni ya Barrick unasimamiwa na Mhandisi Mshauri kutoka TECU Shinyanga na unajengwa na Mkandarasi CCECC kutoka China.

Aidha, barabara hiyo itawekewa jumla ya taa 206 katika miji ya Manzese, Karagwa, Ntobo, Segese, Lunguya, Ilogi, Kakola na Bugalawa ambapo zinatarajiwa kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara nyakati za usiku, kuchochea shughuli za biashara na kuongeza mvuto wa miji hiyo.

Mhandisi Kalando ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutenga na kutoa rasilimali fedha zinazowezesha utekelezaji wa miradi ya miundombinu, akisema kukamilika kwa barabara hiyo kutakuwa na mchango mkubwa katika kukuza Sekta za madini, kilimo na ufugaji.

Ametoa wito kwa wananchi kutunza miundombinu saidizi inayojengwa sambamba na barabara hiyo, ikiwemo taa za barabarani na alama za usalama na uelekezaji wa magari pamoja na watembea kwa miguu, ili iweze kudumu na kuendelea kuwa na tija kwa maendeleo ya Taifa.