Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WATUMISHI WA WIZARA YA UJENZI WAPIGWA MSASA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO


 

Viongozi wa Wizara ya Ujenzi wamepongezwa kwa kuandaa na kutekeleza kwa vitendo mpango wa mafunzo kwa Watumishi wa Wizara hiyo ambapo utekelezaji wake umekuwa ukifanyika kwa awamu ili kuwajengea uwezo watumishi hao katika kutekeleza majukumu yao.

Pongezi hizo zimetolewa Oktoba 15, 2025 na Katibu Tawala Msaidizi, Mkoa wa Arusha, Sehemu ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu, Moses Pesha kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo ambapo amesema ni hatua muhimu na bora ambayo inasaidia kuleta tija katika utendaji kazi wa Wizara au Taasisi.

“Nichukue fursa hii kuipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kuamua kutekeleza mpango huu kwa vitendo kwani wengine huishia kupanga tu na kushindwa kutekeleza”, amesema Pesha.  

Ametoa rai kwa watumishi hao kutumia mafunzo hayo kama chachu ya kuleta mabadiliko chanya katika sehemu zao za kazi yatakayosaidia kuleta maendeleo kwao na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mafunzo hayo kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Henry Godda, ameipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kuandaa utoaji wa mafunzo kwa watumishi wake na kusisitiza Wizara na Taasisi nyingine za Serikali kuiga mfano kutoka Wizara hiyo.

Naye, Mratibu wa Mafunzo hayo kutoka Wizara ya Ujenzi, Afisa Utumishi, Onesmo Mkandawile ameeleza kuwa Wizara imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali kwa watumishi kwa awamu ambapo lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watumishi katika kutekeleza majukumu yao ambapo awamu hiyo ni ya Tatu huku awamu ya kwanza ya mafunzo ikianza mwezi Januari mwaka 2025.