Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WANANCHI WA MABATINI WAPONGEZA MIRADI YA MAENDELEO KATIKA SIKU 100 ZA RAIS SAMIA


WAKAZI wa kata ya Mabatini mkoani Mwanza wamepongeza utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika kata hiyo, ikiwemo ujenzi wa daraja la Mabatini, wakisema imeleta maboresho makubwa ya kiuchumi na kijamii ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza jana wakati wa mahojiano malumu mkazi wa Mabatini, Nyakasama Makore alisema ujenzi wa daraja la Mabatini na uwekaji wa taa za barabarani umesaidia kupunguza athari za mafuriko na kurahisisha shughuli za biashara hususan kipindi cha usiku.

Kwa upande wake, Mariam Samweli, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapelekea mradi wa taa za barabarani, akisema zimepunguza vitendo vya uhalifu na kuwawezesha wananchi kufanya shughuli za kiuchumi hadi nyakati za usiku.

Amesema wanaendelea kushirikiana na Serikali katika shughuli za kijamii ikiwemo kampeni za usafi wa mazingira, huku wakieleza matumaini makubwa ya kuendelea kunufaika na miradi mingine ya maendeleo.

Naye, msimamizi wa mradi wa Mabatini kutoka Nyanza road works, Kulwa Chigugu, alisema kuwa uboreshaji wa miundombinu umeongeza usalama, kurahisisha usafiri na kusaidia wafanyabiashara pamoja na vijana kupata ajira na kipato ambapo ameongeza kuwa kupitia mradi huo wameweza kuajiri wafanyakazi zaidi ya 60.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa daraja na barabara katika kata ya Mkuyuni mradi huo unaendelea vizuri huku mkandarasi akiwa katika hatua za mwisho za kukamilisha mradi huo.

Kwa mujibu wa msimamizi wa mradi,Sefrosa Lyatuu alisema mkandarasi wa mradi huo Jasco Company kwa sasa anajenga mitaro na tayari ameshaweka taa za barabarani katika baadhi ya maeneo ya mradi.

Alisema kabla ya daraja hilo eneo la Mkuyuni lilikuwa linasumbuliwa na mafuriko haswa katika kipindi cha Masika.

“Tunaishukuru Serikali kwa kufadhili na kuendelea kusimamia mradi huu. Barabara na daraja vitasaidia kurahisisha usafiri na kukuza biashara kwa wananchi,”

Kwa upande wake, mmoja ya wanufaika wa mradi huo Charles Ndelema, amepongeza juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu, wakieleza matumaini kuwa kukamilika kwa mradi huo kutachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.