Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WAKANDARASI WANAOCHELEWESHA MIRADI WASIPEWE KAZI NYINGINE: BASHUNGWA


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameuagiza Wakala wa Barabara nchini TANROADS, kuanzia sasa kutowapa kazi Wakandarasi wote wanaochelewesha miradi ya ujenzi na menejimenti zao kuhakikisha wanaripoti ofisini kwake mara moja kwa hatua zaidi.
Amewataka Wasimamizi wa miradi ya barabara  kuwa wabunifu na kusimamia majukumu yao kikamilifu ili kuondoa  changamoto kwa watumiaji wa miundombinu ya ujenzi wa barabara nchini.

Bashungwa amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kukagua athari za mvua, mradi wa mabasi yaendayo kasi awamu ya tatu na miradi mingine ya ujenzi inayoendelea .
Amewaagiza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kuanzia sasa mradi wowote wa barabara unaojengwa nchini katika hatua ya usanifu lazima  washirikiane na taasisi zingine za Serikali ili kuondoa matatizo ya kiutendaji pale ambapo mradi unakamilika na taasisi nyingine inataka kutekeleza mradi wake eneo hilo.

Amesema atakuwa mkali kwa watendaji au Wakandarasi wazembe wanaoshindwa kwenda na kasi ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kusababisha miradi kusuasua.
Bashungwa ameonya tabia ya baadhi ya  wakandarasi kujujilimbikizia miradi mingi kwa wakati mmoja na yote kutotekelezwa kwa kasi inayotakiwa  kimkataba.

"Serikali inapotoa fedha inahitaji huduma kwa haraka hivyo Mameneja nchini kote hakikisheni miradi inakamilika kwa wakati", amesisitiza Waziri Bashungwa

Aidha, Ametoa wito kwa wakandarasi wazawa kufanya kazi kwa bidii ili kuleta tija na kuliwezesha Serikali kuwaamini na kuwapa miradi mingi ili kukuza uchumi wa watanzania.
Nae, Kaimu mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng.  Dorothy Mtenga amesema  ujenzi wa BRT III unaotekelezwa na mkandarasi  Sinohydro unatarajia kukamilila Machi 2024.

"Tumepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali huku akiahidi wataendelea kumsimamia mkandarasi kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kama Serikali inavyotaka katika mradi huo wa BRT awamu ya tatu.

Alikiri kuwa ujenzi wa mradi huo upo nyuma kimkataba ambapo sasa uko asilimia 20 wakati ulitakiwa kuwa asilimia 46.

Meneja Mradi wa kampuni ya Sinohydro, Guo Kun aliahidi kumaliza ujenzi kwa wakati kwani watakuwa wanafanyakazi usiku na mchana.