Habari
UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA MSALATO WAFIKA ASILIMIA 67.6
Kamati ya Ukaguzi ya wizara ya Ujenzi imeridhishwa na kasi ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato mkoani Dodoma ambao umefikia asilimia 67.6 kwa upande wa miundombinu ya njia ya kuruka na kutua ndege huku ujenzi wa jengo la abiria ukifika asilimia 32.21
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhandisi Gilbert Mwoga wakati wa ziara ya ukaguzi ya Kamati hiyo amabapo pamoja na mambo mengine Kamati imesisitiza kuongeza kasi ya ujenzi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.
“Kamati inaendelea kufuatilia mandeleo ya mradi huu kwa ukaribu ili kuhakikisha ubora na vigezo vilivyowekwa na Serikali vinafikiwa licha ya mradi kuwa nyuma kwa asilimia Tatu lakini bado unaendelea vizuri ikiwemo njia ya kuruka na kutua ndege yenye urefu wa Kilometa 3 na mita 600”, amesema Mhandisi Mwoga
Aidha, Mhandisi Mwoga amemshauri Mkandarasi kuendelea kuwa na mahusiano mema na jamii inayozunguka mradi huo kwa kuendelea kutoa huduma kwa jamii kulingana na mahitaji ya jamii husika ili iweze kunufaika kupitia mradi huo.
Kwa upande wake, Mhandisi Mahona Luhende kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS), amesema kuwa mradi huo unajumuisha ujenzi wa jengo la zima moto, Jengo la kuongozea ndege, ujenzi wa maegesho yenye uwezo wa kupokea magari zaidi ya 500, ujezi wa kisima cha kuhifadhia mafuta ya ndege pamoja na jengo la abiria litakalokua na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.2 kwa mwaka.
Kuhusu suala la ajira, Mhandisi Luhende amesema hadi sasa jumla ya wananchi 608 wamepata ajira katika mradi wa ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege huku wananchi 947 wakipata ajira katika mradi wa ujenzi wa jengo la abiria ambapo wageni walioajiriwa ni 31 kwa kila mradi na hivyo kufanya wazawa walioajiriwa katika mradi huo kuwa wengi zaidi.
Ujenzi wa mradi huo unahusisha njia ya kuruka na kutua ndege yenye urefu wa Kilometa 3 na mita 600 ambapo unagaharimu kiasi cha shilingi Bilioni 165.6 pamoja na ujenzi wa jengo la abiria ambalo linagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 194.4