Habari
SERIKALI YAAHIDI KUIUNGANISHA MIKOA YA MBEYA, TABORA NA SINGIDA KWA LAMI.
Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imesema inatafuta chanzo sahihi ili kuweza kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Ipole hadi Rungwa na kufanikisha kuiunganisha Mikoa ya Mbeya, Tabora na Singida kwa kiwango cha lami.
Hayo yamebainishwa Bungeni jijini Dodoma leo, February 02, 2026 na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya wakati akijibu swali la Mbunge wa jimbo la Sikonge Mhe. Amos William Maganga aliyeuliza Serikali ina mpango gani na ujenzi wa barababa ya kutoka Ipole kwenda mpaka Rungwa?
Eng. Kasekenya, amefafanua kuwa barababa hiyo imeshafanyiwa usanifu na ni moja ya barabara kubwa na ambayo haijajengwa kwa kiwango cha lami na hivyo Serikali inatafuta chanzo sahihi cha kwa maana ya kuijenga hiyo barabara.
“Barababa hii imeshafanyiwa usanifu na ni moja ya barababa kubwa ambayo haijajengwa kwa kiwango cha lami na tunavyoongea Serikali inatafuta chanzo sahihi cha kwa maana ya kuijenga barababa hiyo kuanzia Ipole hadi Rungwa na kutoka Rungwa kwenda Singida”, ameeleza Naibu Waziri Eng. Kasekenya.
Amebainisha kuwa tayari Serikali imeanza kujenga sehemu ya barabara hiyo kuanzia Rungwa kwenda Makongorosi ili kuiunganisha Tabora, Singida na Mkoa wa Mbeya kwa kiwango cha lami.
