Habari
ULEGA: TAA 558 KUFUNGWA BARABARA YA NTYUKA - KIKOMBO
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameeleza kuwa Serikali itafunga taa za barabarani 558 katika barabara ya Ntyuka–Mvumi–Kikombo (km 76) inayojengwa kwa kiwango cha lami katika Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma.
Amewahakikishia wananchi wa Jimbo la Mvumi kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama na kuchochea shughuli na fursa mbalimbali za kiuchumi za Mkoa.
Ulega ametoa kauli hiyo wakati akijibu hoja za wananchi katika mkutano wa hadhara ulioongozwa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, uliofanyika jimboni humo.
Amesisitiza uwekaji wa taa hizo ni maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha miradi yote ya barabara inayojengwa inaambatana na usimikaji wa taa za barabarani pamoja na upandaji miti.
Amebainisha kuwa taa hizo zitasaidia kuwezesha shughuli za uzalishaji kufanyika muda wote, usiku na mchana, pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao.
Akizungumzia suala la ajira, Waziri huyo alisema tayari amemuelekeza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Mkandarasi wa mradi kuhakikisha vijana wenye sifa wanapatiwa ajira, huku kipaumbele kikitolewa kwa wakazi wa maeneo yanayopitiwa na mradi.
Sambamba na hilo, Waziri Ulega amemuelekeza Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma kushirikiana na Meneja wa TARURA wa Mkoa huo kuweka taa na matuta yaliyoombwa katika barabara inayoenda Mvumi Mission.
