Habari
ULEGA: MAFURIKO JANGWANI KUWA HISTORIA UJENZI WA DARAJA UKIKAMILIKA
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema mipango ya Serikali kuboresha miundombinu ya jiji la Dar es Salaam ina lengo la kuhakikisha kwamba barabara zote zinapitika mwaka mzima ili kurahisisha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa taifa.
Waziri huyo ametoa maelezo hayo mbele ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, aliyekuwa na ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara jijini Dar es Salaam.
Ulega alitoa mfano wa ujenzi wa Daraja la Jangwani ambapo alisema kukamilika kwake kutaondoa adha ya kukatika kwa njia ya kutoka Magomeni kuelekea katikati ya jiji na kurejea kwa kusema jambo hilo sasa litakuwa historia.
Ameeleza kwamba Daraja la Jangwani lina urefu wa mita 390, upana wa mita 42.8 na kimo cha mita 15, na litakuwa suluhisho la kudumu kwa tatizo la mafuriko katika eneo hilo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likikumbwa na changamoto hiyo wakati wa mvua.
Katika ziara hiyo ya ukaguzi, Ulega alisema maboresho makubwa yanayoendelea jijini Dar es Salaam yanatokana na azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona kwamba miundombinu inakuwa fursa kwa Watanzania badala ya kusababisha kero na ukosefu wa utu kwa wakazi wa jiji hilo.
Kuhusu ujenzi wa miundombinu ya usafiri wa mabasi ya mwendokasi, Ulega ameeleza mradi huo umeleta mapinduzi makubwa kwa wananchi, akibainisha kuwa kwa sasa huduma hiyo inapatikana kuanzia Mbagala hadi Kariakoo ikiwa na mabasi yenye viwango vya kisasa, hali inayorahisisha usafiri na kupunguza adha iliyokuwepo hapo awali.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara, ambapo katika siku chache zijazo baadhi ya maeneo yataanza kuhudumiwa na mabasi ya mwendokasi, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa usafiri jijini humo.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mingine ya kudhibiti mafuriko, ikiwemo mradi wa mifereji katika eneo la Boko Basihaya wenye thamani ya Shilingi Bilioni 57, ambao kwa sasa uko katika hatua ya manunuzi ya kumpata Mkandarasi.
Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa Madaraja ya Mzinga, Mpiji Chini na Ununio, ambayo kwa pamoja inagharimu Shilingi Bilioni 46.5, ikilenga kupunguza na kuondoa kabisa athari za mafuriko katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Mwigulu alikagua miradi ya ujenzi wa Madaraja ya Mkwajuni na Kigogo, ambapo alionesha kuridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa na kwamba hatua zinazochukuliwa zinaonesha mabadiliko makubwa ya maendeleo ya jiji hilo ambao ujenzi wake unagharimu jumla ya Shilingi Bilioni 28.
