Habari
ULEGA: DHAMIRA YA SERIKALI NI KUHAKIKISHA WATANZANIA WANAPATA MAKAZI BORA NA NAFUU
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameeleza dhamira ya Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha watanzania hususan vijana, wanapata makazi bora na ya gharama nafuu kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Majengo (TBA).
Ulega ameyasema hayo jijini Dar es Salaam mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakati ilipotembelea na kukagua miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi ya watumishi wa umma katika eneo la Magomeni Kota Awamu ya Pili pamoja na nyumba za makazi za Canadian Village zilizopo Masaki.
Amebainisha kuwa hadi sasa jumla ya nyumba 174 zinaendelea kujengwa katika eneo la Temeke jijini Dar es Salaam kwa lengo la kusaidia vijana kupata makazi ya gharama nafuu na hivyo kupunguza changamoto ya uhaba wa nyumba katika jiji hilo.
Aidha, Ulega amesema maono ya Rais Samia ni kuhakikisha miradi ya aina hiyo inatekelezwa pia katika majiji mengine nchini kulingana na mahitaji yaliyopo, ikiwemo Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma.
Katika ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Selemani Kakoso, amesema kamati hiyo imeridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo baada ya kufanya ukaguzi na kubaini kuwa ujenzi unaendelea kwa viwango vinavyokubalika na vya kisasa.
Amesema ubora wa nyumba hizo unatokana na ufuatiliaji mzuri unaofanywa na Wizara ya Ujenzi pamoja na Wakala wa Majengo (TBA) katika kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro amesema ujenzi wa mradi wa Magomeni Kota Awamu ya Pili uliofikia asilimia 65 unahusisha majengo matano ya makazi yenye sakafu nane, ambapo kila jengo lina uwezo wa kuchukua familia 16 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni, 2026.
