Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

ULEGA : DARAJA LA MKUYUNI LIMEANZA ‘KULIPA’.


📌 Wananchi wasema bila daraja, maafa yangekuwa makubwa zaidi

📌Asema ni sasa ni mwendo wa kazi na utu tu

 

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la Mkuyuni mkoani Mwanza tayari kumeanza kuonyesha matunda katika siku zake za awali.

Akizungumza na wananchi mara baada ya ukaguzi wa daraja hilo leo Machi 16, 2026, Ulega alisema wakazi wa Mwanza ni mashahidi wa hali hiyo hasa kufuatia matukio ya karibuni ya mvua kubwa zilizonyesha ambapo kama kusingekuwa na daraja, maafa makubwa yangetokea.

“Kwa wastani mvua hapa hunyesha kwa wastani wa milimita 140. Hii ya wiki jana watu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa wanasema kiwango kilikuwa ni milimita 185. Hiki ni kiwango kikubwa ambacho hakijawahi kutokea katika miaka ya karibuni.

"Kuna picha mjongeo zilirushwa kwenye mitandao kuonyesha daraja halijafaa. Hao ni watu wa nje ya Mkuyuni. Watu wa hapa wanajua nini ambacho hili daraja limewafanyia,” alisema Ulega.

Daraja hilo ambalo ujenzi wake ulianza Novemba 2024 na kugharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni tano, ni sehemu ya miradi ya dharura  81 ambayo Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza ijengwe kwa thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 560 ili kuboresha miundombinu iliyoathiriwa na mvua na vimbunga miaka miwili iliyopita.

Katika mkutano huo, Ulega alisema kwamba ni muhimu kwa wananchi kuwa watetezi wa kwanza wa miradi ya serikali kwa kuwajibu watu wanaopotosha ambao kwao serikali haina jambo jema inalowafanyia wananchi.

Ulega alitembelea daraja hilo ikiwa ni sehemu ya maelekezo aliyopewa na Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, kuhakikisha ujenzi wake unakamilika haraka ili kuondoa usumbufu kwa wananchi.

Baada ya ukaguzi wa leo, Ulega alisema sasa atafikisha salamu kwa Waziri Mkuu kwamba kazi hiyo iliyofanywa na mkandarasi mzalendo wa kampuni ya JASCO sasa imekamilika rasmi – ikiwemo ufungwaji wa taa za barabarani.

Katika hatua nyingine, waziri huyo alitoa mchango wa shilingi milioni tano kwa ajili ya kusaidia wafanyabiashara wadogo ambao biashara zao ziliathiriwa na mafuriko ya wiki iliyopita.

“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inajali utu. Nafahamu kwamba hatuwezi kurejesha kila kilichopotea lakini tunachoweza kufanya ni kuonyesha utu kwa wenzetu waliokumbwa na kadhia hiyo,” alisema.

Akitoa taarifa kuhusu daraja hilo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza, Paschal Ambrose, amesema daraja hilo lina upana wa mita 15 na njia sita – nne za magari na mbili za watembea kwa miguu.

Alisema kukamilika kwa daraja hilo kutafungua zaidi njia ya usafiri wa barabara kati ya mikoa ya Mwanza na Shinyanga na kwamba itakuwa na msaada mkubwa hasa katika nyakati za masika ambako eneo la Mkuyuni lilikuwa likifahamika kwa kutopitika.

Akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, alisema wananchi wa Nyamagana wanamshukuru Rais Samia kwa ujenzi wa daraja hilo kwani litakuwa na msaada mkubwa kwao.

Akizungumza kwa mifano, Makilagi alisema kama daraja hilo lingekuwa halipo, huenda hadi leo eneo la Makuyuni lingekuwa halipitiki kwa sababu ya wingi wa maji.