Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

ULEGA AWATAKA WAHANDISI KUENDANA NA MABADILIKO YA AI ILI KUKZA UBUNIFU


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amewataka Wahandisi nchini kuendana na teknolojia ya akili unde ili kukuza ubunifu, ujuzi na kufanikisha Dira ya Tanzania ya 2050.

Akifungua mkutano wa 23 wa Wahandisi jijini Dar es Salam leo Waziri Ulega ametoa wito kwa Wahandisi kukumbatia matumizi ya teknolojia za kisasa, hususan akili bandia (AI), ili kuongeza ubunifu, kupunguza gharama na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Akizungumza katika mkutano huo Ulega amewashukuru washiriki wote kwa kuhudhuria na kuwataka wageni kutoka nchi mbalimbali, wakiwemo Kenya, Uganda na Rwanda, kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya uhandisi na maendeleo ya miundombinu.

Aidha, ameipongeza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), kwa maandalizi ya maadhimisho hayo, akieleza kuwa mkutano huo ni sehemu muhimu ya kujadili nafasi ya taaluma ya uhandisi katika kujenga uchumi wa kisasa na unaotegemea maarifa.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo, “Leveraging Engineering Innovation and Digital Transformation for Sustainable Development,” imeelezwa kuwa ni wito kwa wahandisi kutumia ubunifu na mabadiliko ya kidijitali kama nyenzo muhimu za kutatua changamoto zinazolikabili taifa.

Amesisitiza matumizi ya AI, hayaepukiki kutokana na kasi ambayo dunia inaelekea katika matumizi ya mifumo ya kiotomatiki, roboti, uchambuzi wa data na teknolojia nyingine za kisasa.

 "Badala ya kuiona AI kama tishio kwa ajira wataalam wanapaswa kujifunza namna ya kuitumia kuongeza ufanisi katika kazi zao", amesisitiza Ulega.

Amesisitiza kuwa uhandisi una nafasi kubwa katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, ambayo inalenga kujenga taifa lenye uchumi imara na shindani unaotegemea maarifa, teknolojia, ubunifu, viwanda na rasilimali watu wenye ujuzi.

Miundombinu ya barabara, reli, madaraja, mifumo ya maji, nishati, viwanda, teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na majengo ni sehemu ya safari ya Tanzania kuelekea maendeleo.

Waziri Ulega amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha wahandisi vijana na wanawake ili kuwajengea uzoefu na hivyo kuwa na hazina kubwa ya wataalam nchini.

Nae Msajili wa Wahandisi Eng. Bernard Kavishe amesema zaidi ya Wahandisi 4,000 wameshiriki mkutano huo huku zaidi ya 300 wakila kiapo cha utii.

Ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwaamini wahandisi wazawa  katika ujenzi wa miradi mikubwa ya miundombinu, ikiwemo reli ya kisasa ya SGR na miradi ya nishati. Mradi wa Julius Nyerere Hydropower Station , barabara na madaraja nchini kote.