Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

ULEGA ATANGAZA MSHINDI ‘FOLENI CHALLENGE”


📌Mwanafunzi wa UDSM aibuka kinara

Mwanafunzi wa Shahada ya Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar wa Salaam (UDSM), Tukay Thomas, ameibuka mshindi wa Chemsha Bongo Challenge iliyoanzishwa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega.

Chemsha Bongo hiyo ilianzishwa kama shindano kwa wanafunzi wa shahada za uhandisi katika vyuo vikuu nchini, kwa lengo la kuibua mawazo ya kutatua kero ya foleni nchini.

Kwa ushindi huo, Tukay amepewa zawadi ya shilingi milioni 10, tuzo, kompyuta mpakato na ahadi nyingine katika tukio la utoaji wa zawadi hiyo lililofanyika mjini Dodoma

Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo, Waziri Ulega alisema Wizara imeamua kuwashirikisha vijana katika kutafuta suluhisho za changamoto za usafiri mijini ili kuhamasisha matumizi ya maarifa ya darasani katika vitendo na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya Taifa.

Alisema Tanzania ina wataalamu wa kutosha katika sekta ya miundombinu, jambo linalodhihirishwa na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo reli ya kisasa ya SGR, Bwawa la Kuzalisha Umeme la Mwalimu Julius Nyerere pamoja na ujenzi wa barabara mbalimbali nchini.

“Tumewashirikisha vijana si kwa sababu hatuna wataalamu, bali tunaamini vijana wana nafasi kubwa katika ujenzi wa taifa lao. Tunahitaji mawazo yao, ubunifu wao na nguvu zao kuwa sehemu ya maendeleo ya Tanzania,” alisema Ulega.

Waziri huyo aliwataka vijana kuendelea kuipenda, kuiamini na kuilinda Tanzania huku akiwahimiza kupuuza wanaobeza mafanikio ya Serikali. Alisisitiza kuwa taifa linahitaji kizazi chenye uzalendo, maono na uthubutu wa kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo endelevu.

 

Pia aliwahamasisha vijana walioshiriki mashindano hayo kufungua kampuni zao na kuahidi kuwa Wizara itawasaidia katika mchakato wa usajili kupitia taasisi zake ili waweze kutumia taaluma zao kujijengea uchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.

Awali, Mwenyekiti wa Jopo la Majaji, Arch. Dkt. Daniel Matondo, alisema jumla ya maandiko bunifu 561 yalipokelewa, ambapo 328 yalikuwa ya wanafunzi na 233 hayakuwa na utambulisho. Maandishi hayo yalitoka katika vyuo 38 vya ndani na vyuo vinne vya nje ya nchi. Alisema kati ya maandiko hayo, 176 yalitimiza vigezo na kuingia katika hatua ya uchambuzi wa kina.

Kwa mujibu wa Dkt. Matondo, suluhisho zilizowasilishwa zilionyesha kuwa changamoto ya msongamano wa magari inaweza kutatuliwa kwa mbinu mbalimbali badala ya kutegemea njia moja pekee.

Alisema mapendekezo 19 yaliyoibuka yaligusa maeneo muhimu ya usafiri na mipango miji, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara, usafiri wa umma na matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa trafiki.

Mapendekezo hayo pia yalijumuisha ukamilishaji wa mtandao wa mabasi yaendayo haraka (BRT), ujenzi wa flyover, utenganishaji wa barabara katika maeneo yenye msongamano mkubwa, pamoja na upanuzi wa miundombinu ya usafiri usiotumia magari.

Mapendekezo mengine ni pamoja na kuhamisha baadhi ya huduma nje ya maeneo ya biashara kuu, ujenzi wa barabara za haraka, kuongeza njia katika maeneo yenye msongamano mkubwa, kudhibiti magari makubwa mijini na kuboresha usafirishaji wa mizigo.

Kwa niaba ya wanafunzi washiriki wa Shindano hilo, Rais wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (MUST) Yohana Lucas amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa  kutambua nafasi kubwa ya vijana katika maendeleo ya Taifa na kuthamini dira ya Serikali katika kutengeneza kwa vijana kuchangia mawazo na ubunifu unaoweza kusaidia kutatua changamoto za jamii.

Katika shindano hilo, nafasi ya pili ilichukuliwa na kikundi cha wanafunzi watano kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), waliopata Shilingi milioni tano, huku Godson Jackson kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) akishika nafasi ya tatu na kujinyakulia Shilingi milioni tatu.

Mshindi wa nne alizawadiwa Shilingi milioni mbili, huku washindi wa tano hadi saba wakipata Shilingi milioni moja kila mmoja. Washindi wa nafasi ya nane hadi 10 walizawadiwa Shilingi laki tano kila mmoja. Zawadi nyingine zilizotolewa ni pamoja na kompyuta mpakato (laptop), vyeti na ngao.

Aidha, washindi wa nafasi ya 11 hadi 21 nao walipatiwa kompyuta mpakato pamoja na vyeti vya ushiriki.