Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

ULEGA ATAKA NIDHAMU, UWAZI NA UWAJIBIKAJI SEKTA YA UJENZI


Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, amewataka watumishi wa sekta ya ujenzi na taasisi zake kuongeza uwajibikaji, ufanisi, weledi na nidhamu ya kazi ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa nchini kote inakamilika kwa wakati na viwango vilivyokusudiwa.

Akizungumza Machi 30, 2026 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi, Ulega amesisitiza umuhimu wa taasisi hizo kuwasilisha kwa wakati taarifa za utendaji wa bodi zao ili kuiwezesha Wizara kupanga na kutekeleza mipango yake kwa uhakika na kuleta tija.

"Fanyeni kazi kwa weledi, bidii, maarifa na kuepuka rushwa ili kufikia lengo", amesisitiza Waziri Ulega.

Aidha, Waziri huyo amewataka viongozi wa taasisi za TEMESA, TBA, TANROADS, ERB, CRB, NCC,AQRB,RFB, ICoT na Vikosi vya ujenzi kuongeza kasi ya utekelezaji ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kupata tija.

Katika hatua nyingine Waziri Ulega ameuelekeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuongeza juhudi katika kusimamia miradi ya miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Pia, amezitaka taasisi zinazokusanya maduhuli zikiwemo AQRB, ERB na CRB kuongeza makusanyo pamoja na kudhibiti matumizi ili kuimarisha ufanisi na tija katika taasisi hizo.

Waziri Ulega amewakumbusha viongozi wa Ujenzi kuzingatia maadili ya uongozi wa umma kwa kupiga vita rushwa, kuheshimu utawala wa sheria na kutunza siri za ofisi, akisisitiza kuwa nafasi walizonazo ni dhamana kwa wananchi.

“Ni wajibu wenu kuhakikisha mnasimamia rasilimali za umma kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu ili kuendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwaletea wananchi maendeleo,” amesisitiza Ulega.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Ujenzi ambae pia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi, Mhandisi, Aisha Amour amesema Wizara imejipanga kupitia na kufanyia kazi changamoto zote za watumishi ili kuboresha uhusiano kati ya menejimenti na watumishi ili kuboresha mazingira ya kazi wizarani hapo.

Mkutano wa Baraza la wafanyakazi ulioanza leo utamalizika kesho ambapo pamoja na mambo mengine wajumbe watajadili na kuridhia bajeti ya Wizara ya Ujenzi ya mwaka 2026/2027 kabla ya kuwasilishwa na kusomwa Bungeni.