Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

UJENZI WA DARAJA LA MBWEMKURU NA NANGANO WAENDELEA


Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na ujenzi wa madaraja makubwa ya Mbwemkuru II na Nangano katika eneo la Kibukuta, hatua inayotarajiwa kuondoa changamoto ya mafuriko katika barabara inayounganisha wilaya za Nachingwea na Liwale mkoani Lindi.

Daraja la Mbwemkuru II lina urefu wa mita 64 huku la Nangano likiwa na urefu wa mita 25, na yote yanatekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mpango wa dharura wa CERC (Contingency Emergency Response Component) unaolenga kurejesha na kuimarisha miundombinu iliyoathiriwa na mvua za El-Nino na kimbunga Hidaya kati ya mwaka 2023 na 2024.

Msimamizi wa kazi za ufungaji wa mbao na chuma kwenye daraja la Mbwemkuru II, Joachim Kababa, amesema ujenzi wa madaraja hayo unaendelea vizuri na ukikamilika utaleta afueni kubwa kwa wananchi waliokuwa wakikwamishwa na mafuriko.

Akifafanua zaidi amesema, daraja la zamani liliwahi kufunikwa na maji wakati wa mvua kubwa na kusababisha kukatika kwa mawasiliano kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, dereva wa lori la mizigo, Bw. Idrisa Abdallah, ameipongeza serikali kwa ujenzi wa daraja la Mbwemkuru II akisema litapunguza kwa kiasi kikubwa ucheleweshaji wa bidhaa wakati wa mvua.

 Ameongeza kuwa, madaraja yaliyokuwepo awali yalikuwa hatarishi kwani yakiharibika au maji kuzidi, magari yalilazimika kusimama kwa muda mrefu na kusababisha hasara kwa wasafirishaji.

Barabara inayounganisha Nachingwea na Liwale ni miongoni mwa barabara muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Lindi, hususan katika usafirishaji wa mazao na huduma za kijamii, hivyo kukamilika kwa ujenzi wa madaraja hayo kunatarajiwa kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya mafuriko katika maeneo hayo.