Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

UJENZI WA DARAJA LA J.P MAGUFULI MBIONI KUKAMILIKA, BADO MITA 2 DARAJA KUUNGANISHWA: BASHUNGWA


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amekagua na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa Daraja la J.P Magufuli (Kigongo - Busisi) lenye urefu wa Kilometa tatu linalojengwa kuunganisha barabara kuu ya Usagara - Sengerema - Geita katika Ziwa Victoria ambapo ameeleza bado sehemu ya Mita mbili ili daraja lote liweze kuunganishwa.

Ameeleza hayo leo tarehe 17 Septemba 2024 mkoani Mwanza wakati akikagua Ujenzi wa daraja hilo unaoenda sambamba na ujenzi wa barabara unganishi zenye jumla ya kilometa 1.66 upande wa Kigongo na  Busisi.

“Nimetembea kilometa tatu za Daraja la J.P Magufuli kujionea kazi, nimejiridhisha tumebakiza mita mbili (hatua mbili za miguu), ndicho kipande kilichobaki kukamilisha ujenzi wa kilometa tatu za daraja hili pamoja na barabara za maungio kiliometa 1.66 ambazo pia Ujenzi uanendelea” ameeleza Bashungwa.

Bashungwa amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia maono yake na kuendeleza miradi yote iliyoasisiwa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ambapo ameendelea kutoa fedha ili ujenzi wa Daraja hilo ukamilike kwa wakati na kutoa huduma.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha Mkandarasi analipwa malipo yake ambapo hivi karibuni amepokea shilingi Bilioni 18 ambazo zitamuwezesha kukamilisha ujenzi wa daraja hilo ifikapo mwezi Disemba 2024.

Kadhalika, Bashungwa amempongeza Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS) mkoa wa Mwanza, Mhandisi Mshauri kampuni ya Yooshin Engineering Corporation (Korea) na Mkandarasi Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation ambao wote kwa pamoja wanaendelea kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Bashungwa ameeleza kuwa ujenzi wa daraja hilo umeendelea kutoa fursa kwa Wataalam wa ndani na wahitimu wa kada ya Ujenzi kupata ujuzi na uzoefu ambao utasaidia kupunguza utegemezi wa Wataalam kutoka nje ya nchi.

Aidha, Bashungwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kuendelea kutoa fursa kwa Vijana na Wahitimu waliotoka vyuoni kupata mafunzo kwa vitendo katika ujenzi wa miradi ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa madaraja yaliyoharibiwa na mvua ambapo Serikali imeshatoa shilingi bilioni 840 ya utekelezaji huo.

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa ujenzi wa Daraja la JP Magufuli, Mhandisi Abdulkarim Majuto ameeleza kuwa ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 90.5 na kazi zinaendelea kufanyika usiku na mchana ambapo matarajio hadi kufikia mwanzoni mwa Mwezi Oktoba 2024, Daraja hilo litakuwa limeunganishwa.