Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

TPA WATAKIWA KUJIPANGA UJIO WA MV MWANZA


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Atupele Mwakibete, ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kukamilisha  haraka taratibu za manunuzi ili kuboresha Bandari ya Mwanza North na hatimaye kuruhusu meli kubwa kuweza kushusha na kupakia abiria na mizigo.

 

Ametoa kauli hiyo jijini Mwanza mara baada ya kutembelea Bandari za North na South na kusisitiza kuwa Meli ya MV Mwanza itakapokamilika itaingia ziwani kuanza kutoka huduma hivyo TPA itatakiwa kuboresha bandari za Mwanza, Kemondo na Bukoba kwa kuongeza kina ili kuruhusu meli hiyo kutoa huduma.

 

“Ninafahamu kwa miuondombinu iliyopo haiwezi kuruhusu meli kubwa kutoa huduma katika bandari hizi, kamilisheni taratibu zenu ili MV Mwanza ikikamilika iweze kutoa huduma bila kikwazo chochote", amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.

 

Naibu Waziri Mwakibete ameeleza umuhimu wa Idara ya Masoko ya TPA kusukwa upya kwa ajili ya kuzitangaza Bandari za Ziwa Viktoria ili kuweza kupata mzigo na hatimaye kukuza pato la Mamlaka kupitia mizigo inayosafirishwa kwa kutumia bandari hizo kwa nchi zinazozunguka Ziwa Viktoria.

 

Aidha, Naibu Waziri Mwakibete ameitaka TPA kusimamia miradi inayoendelea kwa kuzingatia thamani ya fedha ili iweze kuwa na matokeo chanya kwa Mamlaka na kwa pato la Taifa.

 

Kwa upande wake Kaimu Meneja Bandari za Ziwa Viktoria, Vicent Stephen, amesema Mamlaka iko kwenye hatua mbalimbali za awali za kuboresha Bandari za Mwanza, Kemondo na Bukoba ili kuweza kuhudumia meli kubwa kama ya MV Mwanza.

 

Kaimu Meneja Stephen ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika bandari za ziwa kwani uwezekezaji huo umeongeza shehena iliyokuwa inahudumiwa kwenye bandari kutoka tani laki 2 na kufikia tani laki 3.

 

Naibu Waziri Mwakibete yuko Mkoani Mwanza kwa ziara ya siku mbili akikagua miundombinu ya Sekta ya Uchukuzi