Habari
TBA YAJA NA SULUHU YA WADAIWA SUGU
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ameupongeza Wakala wa Majengo Nchini (TBA) kwa kuweka mfumo wa kisasa wa kidigitali kwenye kitasa janja (Smart Lock) unaoruhusu mpangaji kuingia ndani kwa kutumia kadi ambayo imeshalipiwa ambapo awali walikuwa wakitumia nguvu na muda mwingi kukusanya kodi kwa wadaiwa sugu.
Amezungumza hayo jijini Arusha, mara baada ya kukagua maendeleo ya jengo la kitega uchumi linalojengwa na Wakala huo ambapo Waziri Profesa Mbarawa amesema jengo hilo litapunguza changamoto za makazi kwa watumishi wanaofanya kazi katika ofisi za Serikali Mkoani humo.
“Mfumo huu ni mzuri sababu ambaye hajalipa hatakuwa na uwezo wa kuingia ndani kwake lakini utawapunguzia sana usumbufu hongereni sana”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Aidha, ameupongeza Wakala huo kwa kukamilisha jengo hilo la ghorofa 10 lenye uwezo wa kuchukua familia 22 kwa kutumia fedha zao za ndani.
“Niwapongeze TBA kwa kuja na mradi huu na nimeridhishwa na hatua iliyofikiwa kwani jengo hili linaendana na thamani ya fedha ambazo zimetumika hapa na, ni matumaini yangu mapato yataongezeka na kuongeza majengo mengine kama haya katika miji”, amesema Prof. Mbarawa.
Naye Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Arusha Eng. Juma Dadi amemweleza Waziri Prof. Mbarawa kuwa mpaka sasa TBA imeshapokea maombi takribani 40 ya wapangaji katika nyumba hizo hali inayowapa motisha ya uhitaji zaidi wa nyumba katika mkoa huo.
Meneja Dandi amesema kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza pato la Wakala na Serikali kwa ujumla kwani idadi ya nyumba zinazomilikiwa na Wakala zimeongezeka na Wakala umetengea fedha ili kujenga nyumba nyingine za biashara kama hizo.
Ameongeza kuwa uwepo wa mradi huo umeweza kuongeza idadi kubwa ya ajira kwa mafundi na wafanyakazi wengine pamoja kuwepo kwa ununuzi mkubwa wa vifaa vya ujenzi.
Jengo la Kitega Uchumi la Makazi mkoani Arusha limegharimu kiasi cha shilingi bilioni 5.5 na kwa sasa limefikia asilimia 98 na linatarajiwa kukumilika mapema mwezi Aprili mwaka huu.