Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

TANZANIA YAJIPANGA UJENZI EXPRESSWAY KIBAHA–CHALINZE–MOROGORO


Tanzania imejipanga kuanza ujenzi wa barabara ya mwendokasi (Expressway) kutoka Kibaha- Chalinze hadi Morogoro, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi, uwekezaji na biashara nchini.

Hatua hiyo imetangazwa kufuatia ziara ya kimafunzo iliyofanyika nchini Korea, ambapo Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega alipata fursa ya kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Maendeleo ya Miundombinu (Global Infrastructure Cooperation Conference – GICC), pamoja na kufanya mazungumzo na taasisi mbalimbali zinazohusika na maendeleo na ufadhili wa miundombinu nchini humo.

Ulega amesema kuwa ujenzi wa Expressway utaenda sambamba na jitihada za kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuimarisha mnyororo wa usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi.

Aidha, alisema miundombinu hiyo itachochea uwekezaji katika viwanda na uzalishaji, kutokana na kupungua kwa gharama na muda wa usafirishaji wa malighafi na bidhaa.

Akieleza kuhusu ziara hiyo, Waziri Ulega amesema kuwa mkutano wa GICC unaofanyika kila mwaka unatoa fursa kwa wadau kutoka mataifa mbalimbali kukutana, kujadili fursa na changamoto za maendeleo ya miundombinu, pamoja na kuweka misingi ya ushirikiano wa kimataifa.

Ameeleza kuwa Tanzania ilitumia fursa hiyo kueleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya miundombinu pamoja na changamoto zilizopo, huku ikieleza namna inavyolenga kuzigeuza changamoto hizo kuwa fursa za uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa kwa manufaa ya Tanzania na washirika wake.

Katika ziara hiyo, Ulega alikutana na viongozi na wataalam kutoka taasisi mbalimbali za Korea, zikiwemo Korea International Cooperation Agency (KOICA), Korea Expressway Corporation, Korea Infrastructure Investment & Development (KIND) na taasisi ya Korea Development Institute (KDI), ambazo zina nafasi muhimu katika maendeleo, ufadhili, usimamizi na tafiti za miundombinu nchini Korea.