Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

TANZANIA NA UTURUKI KUSHIRIKIANA KWENYE MIRADI YA MAENDELEO


Serikali ya Tanzania imeahidi kushirikiana na Nchi ya Uturuki katika  utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ikiwemo Ujenzi wa Chelezo na Meli katika Ziwa Tanganyika.

 

Akizungumza na vyombo vya Habari mjini Ankara Uturuki Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa mara baada ya kukutana na Waziri Uchukuzi na Miundombinu wa Uturuki Adil Karaismailogly amesema utekelezaji mzuri wa mradi wa reli ya Kisasa ya SGR kupitia kampuni ya Yarp Merkezi ya nchi hiyo umechangia Tanzania kuona umuhimu wa mashirikiano kwenye  maeneo mbalimbali ya ushirikiao.

 

“Kampuni ya Yapi Merkezi ni ya nchini uturuki na wanatekeleza mradi wa Reli yetu nchini kwa awamu zaidi ya mbili hiii imetupa hamasa ya kuzungumza nao ili kuona uwezekano wa wao kupata miradi mingine inayotekelezwa na Serikali” Amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

 

Waziri Prof Mbarawa amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi yote iliyojipanga kwa mwaka wa fedha 2022/2023 hasa ile iliyopangwa kutekelezwa katika Ziwa Tanganyika kwa kujenga meli kubwa lengo likiwa ni kuboresha usafiri na usafirishaji nchini na hivyo kuchochea uchumi wa Taifa.

 

Aidha, Prof. Mbarawa ameongeza kuwa meli iliyopangwa kujengwa katika Ziwa Tanganyika inatarajiwa kuwa na uwezo wa kubeba tani elfu tatu, meli ya kubeba Makasha, meli ya abiria 600 pamoja na mizigo tan 400 pamoja na chelezo chenye uwezo wa  chenye uwezo wa kubabeba meli yenye tan elfu tano .

 

Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi na Miundombinu wa Uturuki Adil Karaismailogy amesema kuwa  Serikali ya Uturuki iko tayari kushirikiana  na Tanzania katika kupata makampuni mazuri ya ujenzi wa Meli na chelezo

 

Waziri Prof. Mbarawa yuko nchini uturuki kwa ziara ya siku 3 ya kuzungumza na wawekezaji mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu nchini.