Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

TANROADS YASISITIZWA UBUNIFU NA UWAJIBIKAJI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi, Mhandisi Aisha Amour, amewataka viongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuendeleza ubunifu, weledi na uwajibikaji katika usimamizi wa miradi ya ujenzi na matengenezo ya barabara nchini.

Amesema hatua hiyo ni muhimu ili kutekeleza kwa ufanisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga miundombinu bora na ya kisasa itakayochochea maendeleo ya Taifa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uongozi kwa Menejimenti  ya Wakala huo mkoani Morogoro na Mameneja wa TANROADS wa mikoa yote nchini, Balozi, Mhandisi Amour alisisitiza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza fedha nyingi katika sekta ya miundombinu hivyo wanapaswa kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ubora wa kiwango cha juu na kukamilika kwa wakati.

Aidha, Balozi Mhandisi Amour alieleza kuwa viongozi hao wanapaswa kuendana na kasi ya mabadiliko ya Sayansi na teknolojia duniani, ili kuongeza tija katika sekta ya miundombinu.

“Ni wajibu wenu kuhakikisha rasilimali zinazotolewa na Serikali zinatumika kwa kuzingatia ubunifu,ufanisi, kwa kuzingatia uwazi, matumizi bora na uwajibikaji”, amesema Balozi Amour

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi, Mohamed Besta, alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa taasisi hiyo wa kuimarisha uwezo wa kiutendaji wa maafisa wake waandamizi.

Ameongeza kuwa  mafunzo hayo yatawajengea uwezo zaidi katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa miradi kwa viwango vilivyokusudiwa.

Mhandisi Besta amefafanua kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuongeza maarifa, ufanisi na uwezo wa viongozi wa TANROADS katika kusimamia miradi kwa viwango vilivyokusudiwa, na hivyo kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika utendaji wao wa kazi, hivyo kusaidia Serikali kufikia malengo ya kukuza uchumi kupitia sekta ya miundombinu.